Waziri wa Ulinzi: Maadui wanaogopa jibu kali la Iran
Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema hatua yoyote ghalati ya maadui itaipelekea Jamhuri ya Kiislamu itoe jibu kali na la kuumiza, na ambalo litamfanya adui ajutie.
Brigedia Jenerali Mohammad Reza Ashtiani alitoa indhari hiyo jana Jumanne na kuongeza kuwa, mahesabu yasiyo sahihi ya maadui ndiyo sababu ya kushindwa kwao mbele ya taifa la Iran tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini.
Amesema Jamhuri ya Kiislamu iko imara katika kuimarisha uwezo wake wa kuzuia mashambulizi na kusisitiza kwamba, taifa la Iran hususan Vikosi vyake vya Ulinzi havimuogopi adui yeyote yule.
Brigedia Jenerali Ashtani ameeleza bayana kuwa, taifa la Iran limesimama imara na kishujaa mbele ya maadui ambao hadi hivi sasa wamefeli na wameshindwa kufikia malengo yao.
Amesisitiza kuwa, Vikosi vya Ulinzi vya Iran vina uwezo mkubwa wa ulinzi wa kiistatijia na kuongeza kuwa, Tehran imeweza kuimarisha uwezo wake wa kuzuia mashambulizi kwa kuwatumia vizuri wataalamu wake vijana wenye imani thabiti na kwamba taifa hili litalinda usalama wake bila ya kujali ukubwa wa vitisho vinavyolikabili.
Waziri wa Ulinzi wa Iran ameongeza kuwa, Vikosi vya Ulinzi vya nchi hii vina uwezo wa kutosha wa kudhamini usalama wa taifa na wa nchi zote za eneo hili.
Ikumbukwe kuwa, mnamo Oktoba 9, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aliuonya utawala wa Kizayuni wa Israel na kuuambia kuwa, uvamizi wowote dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu utakabiliwa na jibu kali.