Feb 19, 2024 07:31 UTC
  • Iran yaunga mkono kikamilifu taarifa ya mwisho ya mkutano wa Umoja wa Afrika

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa, inaunga mkono kikamilifu taarifa ya mwisho wa mkutano wa kilele wa wakuu wa Umoja wa Afrika (AU iliyotaka kuhitimishwa jinai za Israel katika Ukanda wa Gaza.

Hayo yameelezwa na Nassir Kan'ani, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye amesisitiza kuwa, taarifa hiyo inaonyesha ni namna gani viongozi na mataifa ya Afrika yanavyofungamana na malengo matukufu ya Wapalestina ya kupigania haki.

Nassir Kan'ani ameongeza kuwa, Iran inatangaza na ina uhakika kwamba kuendelea misimamo hii ya kimisingi na ya ubinadamu na msisitizo wake, sambamba na misimamo ya kutafuta haki na ya kibinadamu ya nchi na mataifa mengi ya dunia katika kuliunga mkono taifa madhulumu la Palestina, kutafanya uwanja huo kuwa finyu zaidi dhidi ya waeneza vita wa Kizayuni na waungaji mkono wake na itakuwa msingi wa kusimamisha vita dhidi ya Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na itapunguza mateso ya watu wa Palestina.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Katika taarifa yao ya mwisho, viongozi katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika uliokuwa ukifanyika mjini Addis Ababa Ethiopia sambamba na kulaani vikali kile walichokiita "hujuma ya Israel" katika Ukanda wa Gaza walitoa mwito kukomeshwa mara moja vita.

Zaidi ya hayo, katika taarifa hiyo, viongozi wa Umoja wa Afrika wametaka uchunguzi huru wa kimataifa ufanyike kuhusu ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu, mashambulizi dhidi ya hospitali, waandishi wa habari na vyombo vya habari, pamoja na matumizi ya silaha  za Israel zilizopigwa marufuku  katika vita dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Tags