May 27, 2024 12:48 UTC
  • Kaimu Rais wa Iran: Tunafungamana na mkakati wetu wa kuimarisha ushirikiano na nchi za Kiislamu

Kaimu Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, taifa hili linafungamana kikamilifu na stratejia na mkakati wake wa kuimarisha ushirikiano wake na mataifa ya Kiislamu.

Muhammad Mokhber amesema hayo katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran Spika wa Bunge la Mali.

Huku akiishukuru serikali na wananchi wa Mali kwa kuonyesha mshikamano wao na serikali na wananchi wa Iran kutokana na msiba wa kuondokewa na Rais wa nchi Ebrahim Raisi  na Waziri wa Mashauri ya Kigeni Amir Abdollahian ameeleza kwamba, ingawa kupoteza  wawili hawa ni jambo gumu na chungu, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bado imeazimia kutekeleza stratijia ya hayati Ebrahim Raisi katika kupanua na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kimataifa hususan na nchi za Kiislamu na zenye msimamo mmoja na Tehran.

Kadhalika Kaimu Rais wa Iran amesema kuwa, kuna udharura wa pande mbili kunufaika na uwezo uliopo baina yao na kueleza kwamba, ana matumaini Mali itavuka salama na haraka kipindi cha sasa na kuwa na usalama na utulivu kamili.

Mazungumzo ya Kaimu Rais wa Iran na Spika wa Bunge la Mali

 

Aidha amesema Iran ipo pamoja na wananchi wa Mali na serikali yao na kwamba, iko tayari kuipatia nchi hiyo ya Kiafrika tajiriba na uzoefu wake katika nyanja mbalimbali.

Kwa upande wake Spika wa Bunge la Taifa la Mali aambamba na kumtakia mafanikio Mohammad Mokhbar katika nafasi yake mpya, ameashiria maslahi na irada ya nchi yake ya kupanua ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kueleza matumaini yake kuwa mchakato wa kupanua ushirikiano wa pande mbili utaendelea.

Tags