Mar 08, 2024 08:08 UTC
  • Iran yaiambia UN: Tuna haki halali ya kujibu vitisho vya Israel

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema Jamhuri ya Kiislamu ina kila haki na uhalali wa kuchukua hatua zote inazoweza kujibu uchokozi na tishio lolote kutoka utawala wa Israel dhidi ya usalama wake wa taifa na maslahi ya nchi hii.

Amir Saeid Iravani amemuandikia barua Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Yamazaki Kazuyuki na Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa umoja huo akisisitiza kuwa, Iran ina kila haki ya kujibu vitisho vya Israel.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amemkosoa vikali Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel kwa kuwasilisha habari za urongo kwa Baraza la Usalama na kutoa madai yasiyo na mashiko dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Amesema madai hayo bandia ya Israel yanalenga kuhalalisha uvamizi wa Wazayuni dhidi ya Lebanon, na kupotosha fikra za waliowengi duniani kuhusu hatua ya utawala huo wa Kizayuni kuendelea kukanyaga sheria za kimataifa na kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Iravani amesema tuhuma hizo zisizo na msingi za Tel Aviv zinalenga kuishughulisha na kuisahaulisha dunia kuhusu kitendo cha Israel cha kuivamia Lebanon na kukanyaga Hati ya Umoja wa Mataifa, na Maazimio Nambari 1559 (2004) na 1701 (2006) ya Baraza la Usalama la UN.

Makombora ya Hizbullah yanayoutia kiwewe utawala wa Kizayuni

Hivi karibuni, Israel Katz, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel aliuambia Umoja wa Mataifa katika barua yake kuwa, eti Iran imeongeza kwa kiwango kikubwa uwasilishaji wa silaha kwa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon.

Hii ni katika hali ambayo, Hizbullah ya Lebanon ilitangaza kuanzisha mashambulizi ya ulipizaji kisasi dhidi Israel baada ya utawala huo wa Kizayuni kuanzisha mashambulizi ya kikatili dhidi ya Wapalestina wa Gaza Oktoba, 2023.

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono haki halali ya Syria na Lebanon ya kujibu vitisho, uchokozi na uvamizi wa Israel dhidi ya uhuru, ardhi na mamlaka ya kujitawala nchi mbili hizo za Kiarabu.

Tags