Iran yawataka Wairaqi waungane ili waweze kuangamiza magaidi wa ISIS
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i10984-iran_yawataka_wairaqi_waungane_ili_waweze_kuangamiza_magaidi_wa_isis
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametoa wito wa kuwepo umoja imara baina ya makundi mbali mbali ya Iraq ili taifa hilo lifanikiwe kuangamiza magaidi wakufurishaji nchini humo na kote katika eneo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 10, 2016 08:39 UTC
  • Iran yawataka Wairaqi waungane ili waweze kuangamiza magaidi wa ISIS

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametoa wito wa kuwepo umoja imara baina ya makundi mbali mbali ya Iraq ili taifa hilo lifanikiwe kuangamiza magaidi wakufurishaji nchini humo na kote katika eneo.

Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo leo Jumapili mjini Tehran katika mkutano wake na Sayyid Ammar Hakim Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq. Ameongeza kuwa Iran itasimama na taifa la Iraq hadi pale magaidi watakapoangamizwa kikamilifu nchini humo.

Zarif aidha amepongeza ushindi mkubwa wa hivi karibuni wa jeshi la Iraq na wanamgambo wa kikabila katika mapigano dhidi ya ISIS au Daesh. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amelaani mfululizo wa hujuma za kigaidi za ISIS nchini Iraq ambapo mamia ya watu wameuawa.

Kwa upande wake Hakima amemfahamisha Zarif kuhusu matukio ya hivi kairbuni nchini humo na kuishukuru Iran kwa kuendelea kuliunga mkono taifa la Iraq katika mapambano yake dhidi ya ugaidi.

Amesema umoja baina ya Jeshi la Iraq na wanagambo wa kikabila ni jambo ambalo lilikuwa na nafasi muhimu katika kukombolewa maeneo kadhaa ya Iraq kutoka mikononi mwa ISIS na kuongeza kuwa magaidi hao wakufurishaji wanakaribia kuangamizwa kikamilifu.