Apr 09, 2024 02:20 UTC

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesema kuwa, nchi yake itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki utakaofanyika mwezi ujao wa Mei.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, Mohammad Eslami alitangaza habari hiyo jana (Jumatatu) na kuongeza kuwa, mkutano huo utafanyika tarehe 5 na 6 za mwezi ujao wa Mei katika mji wa Isfahan wa katikati mwa Iran ili kutoa fursa ya kuangaziwa dhulma linazofanyiwa taifa la Iran katika mradi wake wa amani wa nyuklia.

Jana Jumatatu iliyosadifiana na tarehe 8 Aprili, wananchi wa Iran waliadhimisha "Siku ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia" ambayo imepewa jina hilo kwa ajili ya kuenzi jitihada kubwa za kujivunia za wanasayansi wa nyuklia wa Iran wakati walipokamilisha mchakato wa kuzalisha fueli nyuklia.

 

Tarehe 8 Aprili mwaka 2006, wanasayansi wa Iran walifanikiwa kuzalisha wenyewe kikamilifu fueli nyuklia kwa kiwango cha maabara.

Baada ya mafanikio hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliingia kwenye orodha ya nchi zinazomiliki teknolojia kamili ya urutubishaji urani ambayo ni muhimu mno katika mradi wake wa matumizi ya amani ya nishati ya atomiki. 

Hivi sasa Iran inajivunia kwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha elimu kwenye nyuga tofauti kama uzalishaji kwa wingi wa seli shina, teknolojia ya Nano na katika uzalishaji wa dawa mbalimbali za mionzi ya nyuklia ambazo ni miongoni mwa elimu mpya na za kisasa ulimwnguni.

Tags