IRGC yaikamata meli yenye uhusiano na Israel katika Mlango-Bahari wa Hormuz
Shirika rasmi la habari la Jamhuri ya Kiisamu ya Iran IRNA limeripoti kuwa kikosi maalumu cha wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kimekamata meli ya makontena ya MCS Aries yenye uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel karibu na Mlango-Bahari wa Hormuz.
Mkanda wa video uliotolewa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC unawaonyesha makomandoo wa SNSF wakishuka kwenye rundo la makontena yaliyowekwa kwenye sitaha ya meli hiyo.
Katika mkanda huo wa video, anasikika bahari mmoja wa meli hiyo akisema: “msitoke nje,” kisha anawaambia wenzake waende kwenye eneo la kuendeshea meli huku makomandoo zaidi wa IRGC wakishuka kwenye sitaha.
Ripoti zinasema, taarifa za meli hiyo ya MSC Aries zilipatikana mara ya mwisho karibu na Dubai jana Ijumaa wakati ikielekea Mlango-Bahari wa Hormuz.
Imeelezwa kwamba, meli hiyo ilizima mitambo ya ufuatiliaji wa taarifa zake, ambao ni utaratibu wa kawaida unaotumiwa na meli zenye uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel zinazopita katika eneo hili la Ghuba ya Uajemi.
Tukio hilo limetokea wakati utawala haramu wa Israel ukiwa umejiweka katika hali ya tahadhari kwa kuhofia ulipizaji kisasi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kufuatia shambulio la kigaidi la Aprili Mosi ulilofanya utawala huo wa Kizayuni kwenye jengo la ubalozi mdogo wa Iran katika mji mkuu wa Syria Damascus, na kusababisha vifo vya washauri saba wa kijeshi wa IRGC wakiwemo majenerali wawili.../