Iran yalaani shambulio la kigaidi la Nice, Ufaransa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani mashambulizi ya kigaidi yaliyosababisha vifo katika mji wa Nice nchini Ufaransa.
Bahram Qasimi ameeleza kusikitishwa na mashambulizi hayo ya kigaidi na kusisitiza kuwa ugaidi hauwezi kutokomezwa iwapo hakutakuwepo ushirikiano na jitihada za kimataifa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa upuuzaji wowote na mienendo ya kindumakuwili katika kukabiliana na igaidi, inapaswa kulaumiwa.
Watu wasiopungua 84 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi lililofanyika jana usiku huko Nice baada ya mtu mmoja aliyekuwa ndani ya lori kugonga umati wa watu waliokuwa wamekusanyika katika maadhimisho ya Fataki ya Siku ya Kitaifa ya Bastille.
Katika kipindi cha miezi 18 iliyopita Ufaransa imekumbwa na mashambulizi kadhaa makubwa ya kigaidi yaliyofanywa na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh. Kundi hilo limekiri kuhusika na shambulio la jana mjini Nice.