Iran yaionya Israel dhidi ya 'chokochoko mpya' kuhusu Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i114618-iran_yaionya_israel_dhidi_ya_'chokochoko_mpya'_kuhusu_lebanon
Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametahadharisha dhidi ya chokochoko mpya za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Lebanon kwa kisingizio cha tukio la Majdal Shams katika eneo linalokaliwa kwa mabavu na utawala huo la Golan nchini Syria.
(last modified 2024-07-29T22:57:56+00:00 )
Jul 29, 2024 22:57 UTC
  • Iran yaionya Israel dhidi ya 'chokochoko mpya' kuhusu Lebanon

Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametahadharisha dhidi ya chokochoko mpya za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Lebanon kwa kisingizio cha tukio la Majdal Shams katika eneo linalokaliwa kwa mabavu na utawala huo la Golan nchini Syria.

Akiashiria kauli ya Hizbullah ya Lebanon na vilevile misimamo ya baadhi ya maafisa wa ngazi za juu wa nchi hii ya kukanusha kuhusika kivyo vyote vile Hizbullah katika shambulio la Majdal Shams, Kan’ani amesema: 'Baada ya miezi kumi ya mauaji ya umati huko Ukanda wa Gaza na hasa dhidi ya watoto na wanawake wa Kipalestina, utawala wa kibaguzi wa Israel, umebuni ripoti bandia kwa ajili ya kupotosha fikra za waliowengi duniani na kufunika jinai zake za kutisha huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Shambulio la Majdal Shams katika eneo linalokaliwa kwa mabavu na Israel la Golan nchini Syria

Msemaji huyo wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ameongeza kuwa utawala wa Kizayuni hauna hata sifa ya chini kabisa ya kimaadili ya kutoa maoni na kuzungumzia tukio lililotokea katika eneo la Majdal Shams, na kwamba madai ya utawala huo dhidi ya wengine pia hayatasikilizwa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kutetea uthabiti na usalama wa Lebanon na eneo zima la Asia Magharibi dhidi ya uchokozi wa utawala vamizi wa Kizayuni ni jukumu la jumuiya ya kimataifa hususan Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na akasisitiza kuwa kitendo chochote cha kipumbavu cha utawala wa Kizayuni kinaweza kuvuruga utulivu, usalama na kuwasha moto wa vita katika eneo hili, na kuwa iwapo hilo litathibiti ni utawala huo ndio utakaobeba dhima ya matokeo na taathira za hatua kama hiyo ya kijinga.

Majdal Shams katika eneo linalokaliwa kwa mabavu na Israel la Golan nchini Syria, ilipigwa kwa kombora siku ya Jumamosi, ambapo watu 12 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Kufuatia shambulio hilo, vyombo vya habari na watawala wa Kizayuni wameituhumu Hizbullah ya Lebanon kuwa ndiyo iliyotekeleza shambulizi hilo, tuhuma ambazo zimekanushwa vikali na Hizbullah ikisema haina uhusiano wowote na shambulio hilo katika eneo linalokaliwa kwa mabavu na Israel.

Nasser Kan'ani

Baadhi ya vyanzo vya habari pia vimefichua kuwa chanzo cha tukio la Majdal Shams ni kombora la kutungulia ndege la utawala wa Kizayuni ambalo lilipiga uwanja wa mpira wa miguu katika eneo hilo.

Uongo wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Hizbullah ya Lebanon pia umekabiliwa na majibu ya serikali za eneo na vyama huru vya kisiasa vya Lebanon, ambavyo vimesema kwamba Wazayuni ndio chanzo cha mauaji ya Majdal Shams.

Walid Jumblatt, mkuu wa zamani wa Chama cha Maendeleo ya Kisoshalisti cha Lebanon, amesema tuhuma za utawala wa Israel kuwa ni muqawama wa Lebanon ndio ulirusha kombora huko Majdal Shams ni uongo mtupu. Ameongeza kwamba Hizbullah ni muqawama wa Lebanon na ni sehemu ya Lebanon.

Mohammad Raad, mkuu wa mrengo tiifu kwa muqawama katika Bunge la Lebanon amesema: Uamuzi wowote wa utawala unaoukalia kwa mabavu Palestina wa kuanzisha vita vikubwa dhidi ya Lebanon utaashiria mwisho wa utawala huo.

Viongozi wa utawala wa Kizayuni, kama kawaida yao wanajaribu kukanusha kuhusika na tukio hilo na kulitumia vibaya kwa maslahi yao wenyewe.

Utawala wa kijinai wa Israel, ambao una rekodi nyeusi ya kukiuka haki za binadamu na kuua watu wasio na hatia, mara hii unatumia tukio la Majdal Shams kama chombo cha propaganda kwa ajili ya kupotosha fikra za waliowengi ulimwenguni.

Vita vya Ukanda wa Gaza na jinai za utawala wa Kizayuni katika mauaji ya watoto na wanawake wa Kipalestina vimepelekea waungaji mkono wa amani ulimwenguni kuchukizwa sana na utawala huo haramu.

Watoto wa Gaza; wahanga wakuu wa jinai za utawala wa Kizayuni

Matukio ya eneo na kuendelea vita huko Ukanda wa Gaza kumepelekea kuweko mshikamano na umoja zaidi wa makundi ya muqawama kwa lengo la kukabiliana na utawala wa Kizayuni.

Ndoto ya Wazayuni ya kueneza na kupanua wigo wa vita nchini Lebanon, kwa kutilia maanani utayarifu wa Hizbullah na waungaji mkono wa muqawama wa kukabiliana na uchokozi wa utawala huo, bila shaka litakuwa jinamizi lisilo na kikomo kwa utawala huo wa Kizayuni, Marekani na waungaji mkono wake wengine wa Magharibi.