Aug 31, 2024 11:21 UTC

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Amani na Usalama ya Kimataifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema utawala wa Kizayuni ndicho kikwazo kikuu cha kupatikana uthabiti na maendeleo endelevu katika ulimwengu wa Kiislamu na eneo la Asia Magharibi.

Asadollah Eshragh-Jahromi amesema hayo katika kikao cha 50 cha Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) katika mji mkuu wa Cameroon Yaoundé na kubainisha kuwa, hatua za utawala haramu wa Israel za kuvuruga utulivu ni kikwazo kikubwa cha ushirikiano kati ya nchi za Kiislamu.

Kikao cha 50 cha Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa OIC mjini Yaoundé kilimalizika jana Ijumaa chini ya kaulimbiu "Maendeleo ya Miundombinu ya Uchukuzi na Mawasiliano ndani ya Mfumo wa OIC: Chombo Muhimu katika Mapambano dhidi ya Umaskini na Ukosefu wa Usalama.

Eshragh-Jahromi ameeleza wasiwasi wake mkubwa na kulaani vikali chochoko na jinai za kinyama zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza katika kipindi cha miezi kumi na moja iliyopita,

Aidha ametumia jukwaa hilo kulaani kitendo cha kigaidi cha hivi karibuni cha Israel, cha kumuua Ismail Haniyah, aliyekuwa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas mjini Tehran, akitoa wito kwa jamii ya kimataifa na OIC kuchukua hatua madhubuti kukomesha uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu na mauaji ya halaiki na kuuwajibisha utawala huo kwa jinai zake.

Mwakilishi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ameashiria pia ulazima wa kutiliwa maanani chimbuko la ukosefu wa usalama na kushadidisha mgogoro katika eneo la Asia Magharibi na kusisitiza kuwa, siasa za utawala huo pandikizi ni kikwazo kikubwa cha utangamano baina ya nchi wanachama wa OIC.

Tags