Sep 04, 2024 07:00 UTC
  • Iran yawaita mabalozi wa UK, Australia mjini Tehran

Balozi wa Uingereza mjini Tehran ameitwa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na kukabidhiwa malalamiko ya Jamhuri ya Kiislamu, baada ya serikali ya London kuwawekea vikwazo shakhsia watatu Wairan na taasisi moja ya Iran.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani vikwazo hivyo na kusisitiza kuwa, vinakinzana na matakwa ya serikali mpya ya Uingereza ya kutaka kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu.

Vyombo vya habari vya Uingereza viliripoti siku ya Jumatatu kwamba, watu watatu wa Iran na chombo kimoja wamewekwa kwenye orodha ya vikwazo vya UK kwa madai ya kujihusisha na shughuli zinazoonekana "kuvuruga" usalama wa utawala wa Israel.

Balozi wa Uingereza ametahadharishwa kuwa, uungaji mkono wa nchi za Magharibi kwa mauaji ya kimbari ya Wapalestina na juhudi zao za kumkingia kifua mhalifu wa kivita Benjamin Netanyahu ndio sababu halisi za ukosefu wa uthabiti na usalama katika eneo.

Katika hatua nyingine, Iran imemuita balozi wa Australia mjini Tehran kulalamikia hatua ya ubalozi huo ya kuchapisha kwenye mitandao ya kijamii maudhui ya upotoshaji na inayolivunjia heshima taifa la Iran.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema katika taarifa yake jana Jumanne kwamba, imemuita Ian McConville na kumkabidhi pingamizi kali la Iran kwa maudhui ya dharau iliyochapishwa kwenye ukurasa rasmi wa Instagram wa ubalozi huo juzi.

Iran imelaani vikali uchapishaji wa maudhui hiyo inayokiuka maadili, ikisema maudhui "ya matusi" iliyochapishwa na ubalozi wa Australia ni "kinyume na mila, desturi na utamaduni wa Iran na Uislamu."

Ubalozi wa Australia mjini Tehran ulisambaza kwenye ukurasa wake rasmi wa Instagram maudhui ambayo mbali na kukuza, lakini pia inashajiisha ufuska wa ushoga.

Tags