Iran na Russia katika njia ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili
(last modified Thu, 19 Sep 2024 06:41:42 GMT )
Sep 19, 2024 06:41 UTC
  • Iran na Russia katika njia ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu wa Baraza la Usalama la Shirikisho la Russia kwa madhumuni ya kuboresha mahusiano ya pande mbili.

Masoud Pezeshkian Jumanne wiki hii alikuwa na mazungumzo na Sergei Shoigu Katibu wa Baraza la Usalama la Shirikisho la Russia na akasema serikali ya 14 itaendeleza kwa dhati ushirikiano na hatua zinazoendelea kutekelezwa kwa madhumuni ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi mbili kwa kuzingatia rekodi nzuri ya uhusiano  uliopo baina ya nchi mbili. Rais wa Iran ametaja suala la kukuza na kuimarisha uhusiano kati ya Iran na Russia kuwa limesaidia kupunguza sana athari za vikwazo na hatua zisizo za kiadilifu dhidi ya nchi mbili na kwamba uhusiano kati ya Tehran na Moscow utakuwa  endelevu, wa kudumu na uliostawi.  

Pezeshkian ameashiria matamshi ya Katibu wa Baraza la Usalama la Shirikisho la Russia kuhusu maandalizi ya mkutano wa Marais wa nchi mbili hizo pambizoni mwa Mkutano wa Wakuu wa kundi la BRICS huko Qazan na akasema anatumai kuwa katika mkutano huo, Iran na Russia zitakuwa na mazungumzo chanya na yenye matunda kuhusu ushirikiano wa pande mbili, kikanda na kimataifa na pia katika fremu ya kundi la BRICS, Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai na katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Euro-Asia. 

Sergei Shoigu pia amesisitiza katika mazungumzo hayo kuwa Rais Vladmir Putin wa Russia amemtaka kuwafikishia ujumbe huu viongozi wa ngazi ya juu wa Jamhuri ya Kiislamu kuwa msimamo wa Russia kwa ajili ya kushirikiana na Iran katika masuala mbalimbali ya kikanda haujabadilika. 

Sergei Shoigu

Katibu wa Baraza la Usalama la Shirikisho la Russia wiki hii aliwasili Tehran kwa madhumuni ya kufuatilia mapatano yaliyofikiwa katika safari ya hivi karibuni huko Saint Petersburg ya Ali AKbar Ahmadiyan Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.  

Katika mazungumzo yake na mwenzake wa Iran, Shoigu alitupia jicho makubaliano yaliyofikiwa kati ya Iran na Russia na  akasisitiza kuwa Russia inaunga mkono kwa mara nyingine tena sera ya Iran kuhusu korido na njia za mawasiliano na Jamhuri ya Azerbaijan. 

Katika miaka ya hivi karibuni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia zimekuwa na ushirikiano mkubwa katika  kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika sekta mbalimbali zikiwemo za kiuchumi, kisiasa, kijeshi na kiusalama na mchakato wa ushirikiano kati ya nchi hizi mbili umeongezeka kwa kiasi kikubwa.

Iran na Russia ni wadau wawili muhimu na wenye ushawishi mkubwa katika soko la nishati duniani, ambapo nchi hizi mbili zinaendelea kushirikiana katika sekta hiyo. Wakati huo huo Iran ni moja ya wanachama muhimu zaidi wa OPEC, na huku Russia ikiwa moja ya wauzaji muhimu wa mafuta na gesi katika soko la dunia. Nchi hizi pia zina maliasili tajiri na zina msingi mzuri kwa ajili ya ushirikiano wa pande mbili. 

Uanachama wa Iran na Russia katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai na BRICS kama klabu ya kiuchumi ya madola yanayoibukia pia umekuwa sababu faafu ya ushirikiano mkubwa kati ya nchi hizo mbili katika nyanja mbalimbali. Uwezo mkubwa wa kiuchumi wa Iran umekuwa ni fursa mwafaka kwa Tehran na Moscow kuendeleza ushirikiano wa pande mbili katika miaka ijayo.

Nchi wanachama wa kundi la BRICS 

Iran na Russia pia zimezidisha ushirikiano wa pande mbili kati yao kwa kuzingatia kutekelezwa kwao sera huru na na kukabiliana na hatua za kujitanua na za upande mmoja za Marekani na Magharibi. Vikwazo vya Washington na waitifaki wa Ulaya wa White House vimekuwa msingi wa maelewano makubwa kati ya nchi mbili. Hii ni katika hali ambayo katika sekta ya uchumi ya Iran na Russia pande mbili hizo zimetanguliza mbele sera ya kuachana na matumizi ya dola mkabala wa kutumia sarafu ya taifa ili kukabiliana na uingiliaji wa Marekani na kuzuia athari za vikwazo.

 

Tags