Rais Pezeshkian: Damu ya shahidi Nasrullah itaendelea kuchemka na itasimama wima mbele ya dhulma
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Marekani na waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni wamewaonyesha walimwengu jinsi haki za binadamu, utu wa binadamu na sheria za kimataifa zinavyokiukwa, magaidi na wahalifu wanaitwa watetezi wa haki za binadamu na waungaji mkono wa haki za binadamu kwa wanaodhulumiwa na wanaitwa kuwa ni magaidi.
Rais Masoud Pezeshkian amesema hayo leo alipotembelea ofisi ya Harakati ya Hizbullah hapa mjini Tehran na kusaini kitabu cha kumbukumbu cha shahidi Sayyid Hassan Nasrullah aliyekuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah.
Rais wa Iran ameonyesha kusikitishwa na undumakwili wa madola ya Magharibi na kubainisha kwamba, ulimwengu unapaswa kujua kwamba damu ya shahidi mtukufu, Seyyed Hassan Nasrullah na watu waliokuwa pamoja naye itaendelea kuchemka na itasimama wima mbele ya dhulma.

Wakati wa kuwepo kwake leo katika ofisi ya Hizbullah mjini Tehran, Rais Masoud Pezeshkian, ametoa salamu za rambirambi kwa watu mashujaa wa Lebanon kwa kuuawa shahidi Katibu Mkuu wa Hizbullah, Mujahid mkuu Sayyed Hassan Nasrallah na viongozi wengine wa Hizbullah.
Ikumbukwe kuwa, Ijumaa yatarehe 27 Septemba 2024 Sayyid wa Muqawama, Hassan Nasrullah alifanikiwa kupata daraja ya juu ya kuuliwa shahidi katika jinai ya utawala wa Kizayuni wa Israel na mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya makazi ya raia eneo la Dhahiya, kusini mwa Beirut.
Wakati huo huo, Tume ya Haki za Binadamu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa taarifa ikilaani shambulio la kigaidi la utawala katili na unaotenda jinai wa Kizayuni katika eneo la Dhahiya kusini mwa Beirut, mji mkuu wa Lebanon lililowauwa shahidi shakhsia watajika wa muqawama pamoja na mujahid Sayyid Hassan Nasrullah Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon.