Balozi wa Iran UN: Tuhuma za Marekani na Uingereza hazina msingi wowote
Nov 23, 2024 07:21 UTC
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amekanusha tuhuma dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu zilizotolewa na Marekani na Uingereza za eti kuvuruga amani katika eneo la Asia Magharibi na kuhusika na mapigano yanayoendelea Ukraine; akisisitiza kuwa tuhuma zote hizo hazina msingi wowote.
Amir Saeed Iravani amesema katika barua aliyomuandikia Barbara Woodward, Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, Marekani na Uingereza haziwezi haziwezi kujivua na dhima wakati ndizo zinazofanikisha jinai zinazofanywa na utawala wa Israel, kwa sababu uungaji mkono wao usio na masharti kwa Tel Aviv umechochea kuendelea kwa mapigano na kudhoofisha utekelezwaji wa jukumu la Baraza la Usalama la kudumisha amani na usalama kimataifa.
Iravani ameeleza kuwa, badala ya kuhimiza amani na usalama, Marekani imelidumaza Baraza la Usalama na kuupa kibali utawala wa Israel kuendeleza kwa kinga kamili hujuma na mauaji kwa kisingizio cha kujilinda na akaongezea kwa kusema: "suala hili muhimu linaonekana wazi katika kura ya turufu dhidi ya azimio la kusitisha mapigano iliyopigwa hivi karibuni na Marekani".
Kadhalika, Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kwa kusema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakanusha vikali tuhuma zinazofanana na hizo zilizotolewa na Marekani na Uingereza dhidi ya Iran kuhusiana na mapigano nchini Ukraine, ambazo zilitolewa katika kikao cha wazi cha Baraza la Usalama chini ya ajenda ya "kudumisha amani na usalama wa kimataifa nchini Ukraine" na inatangaza kuwa msimamo wake kuhusiana na Ukraine uko wazi, thabiti na haujabadilika.
Mnamo Agosti 30, 2024, Umoja wa Mataifa ulifanya kikao chini ya mada "Vitisho dhidi ya amani na usalama wa kimataifa", ambao ulihusu utumaji silaha wa Magharibi kwa Ukraine.
Katika kikao hicho, wawakilishi wa Marekani, Uingereza na Ufaransa kwa mara nyingine waliratibu madai yanayofanana dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na mzozo unaoendelea nchini Ukraine. Wawakilishi wa Ufaransa na Uingereza walitoa madai yao yasiyo sahihi kimakosa kwa kutegemea Azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (2015), huku mwakilishi wa Marekani, mbali na kukariri madai hayo hayo ya uwongo, aliishutumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa eti inaunga mkono ugaidi.../