Jeshi la Iran laanza Luteka ya Zulfiqar-1403 pwani ya kusini
(last modified Sat, 22 Feb 2025 11:52:46 GMT )
Feb 22, 2025 11:52 UTC
  • Jeshi la Iran laanza Luteka ya Zulfiqar-1403 pwani ya kusini

Vikosi tofauti vya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimeanza awamu kuu ya mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya Zulfiqar-1403 leo Jumamosi (Februari 22) katika pwani ya Makran, kusini mashariki, Bahari ya Oman, na kaskazini mwa Bahari ya Hindi.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, kikosi cha askari waendao kwa miguu, vitengo vilivyo na silaha na mitambo, mifumo ya ulinzi, vikosi vya majini, na vyombo vya juu na chini ya maji vipo katika eneo hilo la maneva ya kijeshi kusini mwa nchi.

Kwa kuanza awamu kuu ya luteka hiyo, vitengo hivyo vimeanza kufanya mazoezi mbalimbali kwa wakati mmoja. Admeli Habibollah Sayyari, Naibu Mratibu Mkuu wa Jeshi la Iran na kamanda wa mazoezi hayo, amesema kuwa maneva hayo yanalenga kuimarisha uwezo wa kiulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu na uwezo wa kuzuia hujuma za vitisho vyovyote vya ardhini, angani na baharini.

Kamanda huyo ameonya kwamba, adui yeyote anayefikiria kudhuru mamlaka ya kujitawala au maslahi ya Iran, iwe ardhini, angani, au baharini, bila shaka atakabiliwa na madhara makubwa.

Admeli Habibollah Sayyari, Naibu Mratibu Mkuu wa Jeshi la Iran

Admeli Sayyari amebainisha kuwa, mazoezi hayo yanalenga kupima zana na mbinu mpya zilizobuniwa na kizazi cha vijana ndani ya Jeshi la Iran. Kwa mujibu wa kamanda huyo, luteka hiyo inajumuisha silaha za hali ya juu, silaha erevu, zilizo sahihi na zinazoongozwa na kuelekezwa tokea mbali, na vile vile aina mbalimbali za makombora.

Mazoezi hayo pia yanatathmini utayarifu wa teknolojia kama vile vita vya mtandao na kielektroniki, ambavyo vina uwezo wa kutathmini upya uwanja wa vita siku zijazo.

Brigedia Jenerali Alireza Sheikh, msemaji wa mazoezi hayo amesema kuwa, helikopta za Kikosi cha Cobra pamoja na helikopta za RH, SH, na AB-212 zimepaa na kutua kwenye manowari za Jeshi la Wanamaji kwenye luteka hiyo.