Araqchi: Tunachotegemea kwa Ulaya ni kulaani mashambulizi ya Israel
(last modified Sat, 14 Jun 2025 02:24:38 GMT )
Jun 14, 2025 02:24 UTC
  • Araqchi: Tunachotegemea kwa Ulaya ni kulaani mashambulizi ya Israel

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa: Serikali na wananchi wa Iran wanataraji kuiona jamii ya kimataifa hususan Umoja wa Ulaya unalaani shambulio hilo la kijinai la Israel dhidi ya nchi yao.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, amezungumza kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Antonio Tajani, na ametilia mkazo hatua zinazopaswa kuchukuliwa na jamii ya kimataifa na hasa nchi za Ulaya kuhusu uchokozi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya vituo vya nyuklia na mashambulizi katika maeneo ya makazi raia na mauaji ya maprofesa wa vyuo vikuu, maafisa wa ngazi za juu wa kijeshi na watu wasio na hatia nchini Iran akisisitiza kuwa, linachotarajia taifa la Iran ni kuona jinai hizo za Israel zinalaaniwa kimataifa na hasa Umoja wa Ulaya.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, jibu la Iran kwa uchokozi wa utawala ghasibu wa Israel litakuwa la uhakika na kali sana.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia amesisitiza kwamba, alikuwa amewajulisha maafisa wa Israel kwamba hatua yao hiyo haikubaliki na lazima ikomeshwe.

Antonio Tajani, metoa mwito wa kujizuia na kutangaza kuwa tayari Italia kufufua njia ya mazungumzo ya kurejesha amani na utulivu katika eneo hili.