Shamkhani: Baadhi ya nchi ajinabi haziko tayari kupatiwa ufumbuzi suala la Daesh
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i12934-shamkhani_baadhi_ya_nchi_ajinabi_haziko_tayari_kupatiwa_ufumbuzi_suala_la_daesh
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ametaka kuwepo umoja na mshikamano baina ya jamii na makundi mbalimbali kwa ajili ya Iraq moja.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 09, 2016 08:52 UTC
  • Shamkhani: Baadhi ya nchi ajinabi haziko tayari kupatiwa ufumbuzi suala la Daesh

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ametaka kuwepo umoja na mshikamano baina ya jamii na makundi mbalimbali kwa ajili ya Iraq moja.

Ali Shamkhani amesema kuwa kuliangamiza kundi la Daesh huko Iraq itakuwa hatua nzuri katika kuleta mshikamano na kuimarisha utambulisho wa kitaifa nchini humo; na ni kwa sababu hiyo ndio maana baadhi ya pande za nje hazitaki kuona suala la Daesh likipatiwa ufumbuzi.

Ali Shamkhani ameyasema hayo leo Jumanne katika mazungumzo hapa Tehran na Barham Saleh Naibu Katibu Mkuu wa Muungano wa Patriotic Union of Kurdistan (PUK) wa Iraq.

Ali Shamkhani kulia akipeana mkono na mgeni wake Barham Saleh mjini Tehran

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema nembo muhimu zaidi ya utendaji wa serikali yoyote ile ni uwezo wake wa kupambana na vitisho vikuu vya kiusalama na kuongeza kuwa, suhula na uwezo huo ambao leo hii umeandaliwa huko Iraq kupitia marajii wa kidini, ushupavu wa vikosi vya jeshi, vikosi vya kujitolea vya wananchi na sera zinazotekelezwa na serikali, unaonekana kuwa matarajio tu katika nchi nyingi katika eneo zinazodai kupambana na Daesh.

 

Magaidi wa Daesh wanaotenda jinai na hujuma mbalimbali huko Iraq

Shamkhani ameshiria pia uhusiano wa siku nyingi na mzuri kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na makundi ya Wakurdi huko Iraq na kuongeza kuwa urafiki mkubwa kati ya Iran na ndugu zao wa Kikurdi umepelekea kuwepo ushirikiano na mapambano ya pamoja kwa miaka kadhaa mtawalia katika medani ngumu na zilizojaa mivutano; uhusiano ambao hauwezi kuvunjika.

Naibu Katibu Mkuu wa Muungano wa Patriotic Union wa Kurdistan ya Iraq pia amesifu na kupongeza hatua kubwa na uungaji mkono endelevu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mapambano dhidi ya ugaidi na kusisitiza kuwa kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Iran ni jambpo lenye umuhimu wa kipekee kwa eneo la Kurdistan huko Iraq.