Pezeshkian: Iran, Belarus zimesimama kidete kukabiliana na ubeberu wa US
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amesema Marekani na baadhi ya washirika wake wa Magharibi wanalenga kupanua ubeberu na msimamo wa upande mmoja duniani kote, sambamba na kuyaburuza mataifa mengine, akisisitiza kwamba si Iran wala Belarus itavumilia muenendo huo.
"Hii leo, Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya zinajaribu kueneza msimamowa upande mmoja na kuzitwisha nchi nyingine mitazamo yao kwa. Mtazamo kama huo haukubaliki na hautavumiliwa na nyinyi wala na sisi," Pezeshkian amesema hayo katika mazungumzo na mwenzake wa Belarus, Alexander Lukashenko huko Minsk leo Jumatano.
Pezeshkian aliwasili katika mji mkuu wa Belarus leo Jumatano kufuatia ziara ya Armenia. Ziara yake rasmi ya siku mbili inalenga kuimarisha uhusiano wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni wa pande mbili.
"Nchi za Magharibi, zikiongozwa na Marekani, zinatafuta kutengeneza njia yetu kwa mujibu wa matakwa yao wenyewe. Hata hivyo, Iran na Belarus zinaamini kuwa, zinaweza kusimama dhidi ya nchi zinazotaka kuzishinikiza nchi nyingine kwa vikwazo, na kwamba zinaweza kuondokana na vikwazo na matatizo mengine kwa kuwa na ushirikiano," Rais wa Iran amebainisha.
Pezeshkian amepongeza uhusiano wa kirafiki wa pande mbili kati ya Iran na Belarus, na kusema kwamba nchi hizo mbili zina misimamo sawa juu ya masuala mengi ya kikanda na kimataifa, na zina ushirikiano madhubuti katika nyanja za kimataifa.
"Zaidi ya hayo, Jumuiya ya Kiuchumi ya Eurasia, Shirika la Ushirikiano la Shanghai, na BRICS zinaweza kutumika kama mifumo na majukwaa ya kuwezesha ushirikiano kati ya Iran na Belarus," amebainisha Dakta Pezeshkian.
Kwa upande wake, Lukashenko ameielezea Belarus kuwa nchi rafiki na mshirika wa kutegemewa wa Iran. Kabla ya kuitembelea Belarus, Rais wa Iran aliizuru Armenia na kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo.