Iran yalipiza kisasi: Balozi wa Australia aondoka Tehran
-
Ismail Baqaie
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ametangaza kwamba balozi wa Australia mjini Tehran ameondoka nchini na kuongeza kuwa: "Kwa mujibu wa kaida na sheria za kidiplomasia, katika kukabiliana na hatua ya Australia ya kumfukuza balozi wa Iran mjini Canbera, Jamhuri ya Kiislamu imejibu mapigo kwa kupunguza kiwango cha uhusiano wa kidiplomasia wa Australia nchini Iran."
Ismail Baqaie, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, amedokeza kwamba hatua ya serikali ya Australia kupunguza kiwango cha uhusiano wa kidiplomasia na Iran haina msingi, akisema: "Hatufurahii kupunguzwa kiwango cha uhusiano, kwa sababu tunaamini hakuna sababu au uhalali wa jambo hili, na linaathiri uhusiano kati ya mataifa mawili."
Baqaei amesisitiza kwamba ubalozi wetu mdogo huko Canberra unafanya kazi, amesema: "Licha ya vizuizi vilivyowekwa kwa ubalozi wetu, tunajaribu kutoa huduma muhimu za kibalozi kwa Wairani wanaoishi Australia."
Amemalizia kwa kusema: "Tuhuma za chuki dhidi ya Uyahudi zilizotolewa dhidi ya Iran ni za kipuuzi na zisizo na msingi."
Mwezi uliopita, Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese aliishutumu Iran kuwa ilipanga mashambulizi mawili kwenye maeneo ya Wayahudi mwezi Oktoba na Desemba, madai yaliyotolewa bila kuwasilisha ushahidi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alilaani uamuzi huo na kusema ni kitendo cha kutaka kuiridhisha "serikali inayoongozwa na wahalifu wa kivita."
Iran pia iliapa kuchukua hatua zinazofaa za kulipiza kisasi baada ya Australia kumfukuza balozi wa Jamhuri ya Kiislamu nchini humo kwa madai ya "chuki dhidi ya Wayahudi," na kusisitiza kwamba vitendo vya ubaguzi wa kidini havina nafasi katika utamaduni, historia au imani ya taifa la Iran.