Araqchi: 'Iran itaendelea kuunga mkono Muqawama wa Palestina dhidi ya Israel'
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i130434-araqchi_'iran_itaendelea_kuunga_mkono_muqawama_wa_palestina_dhidi_ya_israel'
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesisitiza dhamira ya nchi hiyo ya kuunga mkono Muqawama halali na mapambano ya watu wa Palestina dhidi ya utawala vamizi wa Israel hadi pale haki zao zitakaporejeshwa kikamilifu.
(last modified 2025-09-05T03:37:24+00:00 )
Sep 05, 2025 03:37 UTC
  • Araqchi: 'Iran itaendelea kuunga mkono Muqawama wa Palestina dhidi ya Israel'

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesisitiza dhamira ya nchi hiyo ya kuunga mkono Muqawama halali na mapambano ya watu wa Palestina dhidi ya utawala vamizi wa Israel hadi pale haki zao zitakaporejeshwa kikamilifu.

Abbas Araqchi alitoa maoni haya jana Aklhamisi alipokutana na wajumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya harakati ya Hamas huko Doha, nchini Qatar.

Vilevile amekutana na Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, Amir wa Qatar, ambapo majadiliano yalijikita katika kuimarisha uhusiano wa pande mbili za Iran na Qatar na kushughulikia masuala ya kieneo na kimataifa, hususan mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala wa Israel katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Araqchi ameashiria udharura wa nchi za kieneo na jamii ya kimataifa kuchukua hatua za pamoja za kukomesha mauaji ya kimbari, kuwafungulia mashitaka wahusika na kukabiliana na uchochezi na ukatili wa utawala ghasibu wa Israel.

Ameashiria kuongezeka ukatili na machafuko huko Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, ikiwa ni pamoja na kulazimisha njaa watu wasio na hatia wa Gaza na mauaji ya wanawake na watoto kwenye safu za usambazaji wa chakula.

Ameeleza kuwa maandamano makubwa yanayofanyika duniani kote kupinga ukatili huo yanadhihirisha mwamko wa kimataifa kuhusu mgogoro wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran ametoa wito wa kuwepo juhudi zilizoratibiwa kati ya mataifa ya Kiislamu kukomesha mauaji ya kimbari huko Gaza, kuwasilisha misaada ya kibinadamu kwa wale walioathirika, na kuwawajibisha viongozi wa Israel kwa uhalifu wao.

Kwa upande wake, Khalil al-Hayya, kiongozi wa Hamas huko Gaza, amepongeza misaada na uungaji mkono wa Iran kwa kadhia ya Palestina, akisisitiza kwamba jinai za Israel hazitazima azma ya Wapalestina ya kupigania na kutetea haki zao.