"Hatua ya nchi za Ulaya kuamilisha utaratibu wa snapback ni ya kiholela"
Khatibu wa Muda wa Swala ya Ijumaa iliyoswalia leo hapa Tehran amesema: Kwa mujibu wa taarifa ya mwisho ya Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, jaribio lolote la kubadilisha Azimio Nambari 2231 linadhoofisha itibari ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na kwamba hatua ya nchi tatu za Ulaya ya kuamilisha utaratibu wa "snapback" wa kurejesha vikwazo vya baraza hilo dhidi ya Iran ni ya kiholela.
Katika hotuba zake za Swala ya Ijumaa mjini Tehran leo, Hujjatul Islam Sayyid Muhammad Hassan Abu Turabi Fard amesema: "Kubadilisha kiholela azimio hilo kunadhoofisha uaminifu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa."
Amelaani hatua ya Ufaransa, Ujerumani na Uingereza ya kuanzisha mchakato huo wa kuanzisha utaratibu wa kurejesha vikwazo vya Baraza la Usalama dhidi ya Iran (snapback) kutokana na mpango wake wa nyuklia, akiitaja kuwa ni haramu, ya kisiasa na iliyotekelezwa kwa mashinikizo ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Hujjatul Islam Abu Turabi Fard amesema: Tuko mwanzoni mwa Wiki ya Umoja, siku tukufu na adhimu za kuzaliwa Mtume Mtukufu wa Uislamu. Jua lililochomoza katika ardhi ya Hijaz na kuuangazia ulimwengu wa ubinadamu kwa nuru ya Wahyi.
Ameeleza kuwa, "Kwanza ninarejelea ubora wa hali ya juu wa Manabii wa Allah, falsafa ya uumbaji wa mwanadamu na ulimwengu, na njia ya kufikia kilele ambacho Mwenyezi Mungu ametayarisha kwa ajili ya mwanadamu na jamii za wanadamu."
Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran ameongeza kuwa: "Lengo tukufu la ujumbe wa Manabii wa Mwenyezi Mungu ni kujenga mfumo wa kisiasa na jamii wa wanadamu unaozingatia uadilifu, ili jamii ya mwanadamu iweze kufikia kilele cha elimu na ubora."
Akiashiria kwamba bendera ya juu kabisa iliyoinuliwa na Quran ni bendera ya sayansi, Hujjatul Islam Sayyid Muhammad Hassan Abu Turabi Fard amesema: "Miaka 1400 iliyopita, wakati jamii za wanadamu hazikujua kuandika sayansi, Quran iliinua bendera hii. Njia hiyo inayompeleka mwanadamu kwenye heshima ya utu ni njia ya mantiki na ya sayansi."