Araqchi: Nchi 3 za Ulaya lazima zibadili njia yao ya uharibifu
-
Sayyid Abbas Araqchi
Katika makala yake kwenye gazeti la The Guardian, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema kwamba nchi tatu za Ulaya (Ufaransa, Uingereza na Ujerumani), zinapaswa kubadili mkondo wao wa uharibifu, akisisitiza kuwa: "Mchezo huu hautakuwa na matokeo yanayotarajiwa kwa nchi hizo, bali utakuwa na matokeo kinyume na utasababisha kutengwa zaidi kwa nchi hizo tatu kwa kuziondoa katika diplomasia ya baadaye."
Sayyid Abbas Araqchi ameandika makala hiyo katika gazeti la The Guardian la Uingereza kufuatia hatua ya nchi hizo tatu za Ulaya ya kutuma barua kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kuanzisha utaratibu wa kurejesha vikwazo vya baraza hilo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu maarufu kama snapback mechanism.
Akieleza kwamba Ulaya imekuwa katikati ya mgogoro uliobuniwa na unaoendelea kuhusu mpango wa amani wa nyuklia wa Iran kwa zaidi ya miongo miwili, anaandika kwamba: "Ulaya, ambayo hapo awali ilikuwa nguvu ya kuweka mlingano ilikuwa na nia ya kudhibiti Marekani mchochea vita, leo imekuwa sababu ya kuimarisha sera za kupenda makuu na kujipanua za Washington.."
Araqchi, ameeleza kuwa wiki iliyopita nchi tatu za Ulaya (Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani) zilitangaza kuwa zimeanzisha mchakato wa kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran (snapback), na kuongeza kuwa: Utaratibu huu ulibuniwa ili kuadhibu "upande ambao hautatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia ya 2015 (JCPOA). Lakini mienendo ya hivi majuzi ya Ulaya haina msingi wowote wa kisheria, kwani inapuuza msururu wa matukio yaliyopelekea Iran kuchukua hatua za kufidia hasara zilizosababishwa na kutotekeleza majukumu upande wa pili.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran ameongeza kuwa: "Nchi hizo tatu za Ulaya zinataka walimwengu wasahau kwamba ni Marekani - na si Iran - ndiyo iliyojiondoa kwa upande mmoja katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Nchi hizo tatu za Ulaya pia zinataka watu wasahau kutotekeza kwao majukumu yanayotokana na makubaliano hayo na uungaji mkono wao wa kuaibisha kwa mashambulizi ya mwezi Juni mwaka huu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu."
Araqchi amesema kuwa: Rais Donald Trump wa Marekani ameonyesha wazi kwamba anazitambua nchi hizo tatu za Ulaya (Uingereza, Ufaransa na Ujerumani) kuwa ni wahusika wa pembezoni, na ukweli huu umethibitika kwa kuiweka kando Ulaya katika masuala muhimu yanayoihusu, ukiwemo mzozo wa Russia na Ukraine.