Iran kurusha satelaiti tatu mpya katika anga za mbali
Iran iko mbioni kupiga hatua kubwa katika mpango wake wa anga za mbali kwa kuzindua satelaiti tatu mpya ambazo ni Kowsar, Zafar, na Paya kabla ya mwisho wa mwaka wa Kiirani (tarehe 20 Machi, 2026).
Hayo ni kwa mujiibu wa taarifa ya Hossein Salariyeh, mkuu wa Shirika la Anga za Mbali la Iran (ISA). Akizungumza na Tasnim News, Dkt. Salariyeh amesema uzinduzi wa satelaiti hizo unatarajiwa kuimarisha uwezo wa Iran katika teknolojia ya satelaiti.
Amesema satelaiti ya Kowsar ina mifumo ya kisasa ya picha za anga (high-resolution imaging), na itatumika katika kilimo, mipango ya miji na ufuatiliaji wa mazingira. Nayo satelaiti ya Zafar imeundwa kuboresha mitandao ya mawasiliano, hasa katika maeneo ya mbali yasiyofikiwa kirahisi. Halikadhalika satelaiti ya Paya itajikita katika ufuatiliaji wa hali ya hewa na maandalizi ya kukabiliana na majanga ya asili.
Mbali na satelaiti hizo tatu, Dkt. Salariyeh amefichua mpango wa Nahid 2, jukwaa la mawasiliano ya bendi nyembamba litakalopanua upatikanaji wa intaneti katika maeneo yasiyo na huduma bora.
Pia amedokeza kuhusu mfumo mpya wa satelaiti wa Shahid Soleimani, ambao ni mkusanyiko wa satelaiti utakaowezesha muunganisho wa mawasiliano wa kudumu na wa kuaminika.
Amesema: “Mfumo huu ni hatua kubwa kuelekea kwenye kujitegemea katika teknolojia ya anga."
Tangazo hili linaashiria dhamira ya Iran kuimarisha nafasi yake katika utafiti wa masuala ya anga, wakati dunia ikiendelea kusonga mbele kiteknolojia.
Wanasayansi na wahandisi wa Iran wanafanya kazi kwa bidii kuhakikisha kunapatikana mafanikio ya operesheni hizo za kutuma satelaiti katika anga za mbali, ambazo zinatarajiwa kutoa data muhimu na huduma za kiteknolojia.
Iran hivi sasa ni miongoni mwa nchi 10 za dunia zenye uwezo mkubwa katika anga za juu, mafanikio ambayo yamepatikana kutokana na juhudi za zaidi ya miongo 4 za wataalamu wa hapa nchini, na kwa hivyo Iran ina nafasi muhimu katika sekta hii kati ya nchi chache zilizo na teknolojia hiyo.