Iran yaripoti kuongezeka biashara na nchi za Afrika
Iran imetangaza ongezeko kubwa la mauzo ya bidhaa nje ya nchi kuelekea bara la Afrika, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kupanua masoko ya biashara na kupunguza utegemezi wa mauzo ya moja kwa moja ya mafuta ghafi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya Iran ya Biashara, Viwanda, Madini na Kilimo (ICCIMA), mauzo ya Iran kwenda Afrika yaliongezeka mara 2.2 katika kipindi cha miezi minne iliyoishia Julai, ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Idara hiyo imenukuu taarifa ya Masoud Barahman, mfanyabiashara wa ngazi ya juu anayesimamia biashara kati ya Iran na nchi za Afrika, akieleza kuwa mauzo hayo yamepanuka katika miezi mitano iliyopita na kuingia kwenye masoko mapya.
Barahman amefafanua kuwa idadi ya nchi za Afrika zinazoagiza bidhaa zisizo za mafuta kutoka Iran imeongezeka kutoka 29 mwezi Machi hadi kufikia 34 mwezi Julai.
Ameongeza kuwa mauzo hayo yanatarajiwa kuendelea kuongezeka katika miezi ijayo kutokana na kuimarika shughuli za usafirishaji na kupunguzwa vikwazo vya forodha.
Takwimu zilizotolewa na Idara ya Forodha ya Iran mwezi Julai zinaonesha kuwa mauzo ya Iran kwa nchi za Afrika yaliongezeka kwa asilimia 85 mwaka hadi mwaka katika kipindi cha miezi mitatu hadi mwishoni mwa Juni, na kufikia zaidi ya dola milioni 260.
Iran iliwaalika maafisa wa serikali na viongozi wa biashara kutoka nchi kadhaa za Afrika kushiriki katika mkutano mkubwa wa ushirikiano wa kiuchumi uliofanyika Tehran mwishoni mwa Aprili.
Mkutano huo uliipa Iran fursa muhimu ya kupanua masoko yake ya bidhaa barani Afrika, ambako inatarajia kuimarisha ushawishi wake wa kiuchumi katika siku za usoni.
Mpango wa Iran wa kupanua uhusiano wa kibiashara na Afrika unaendana na juhudi za kitaifa za kubadilisha muundo wa uchumi wake na kupunguza utegemezi wa mapato yanayotokana na mauzo ya mafuta.