Aragchi: Ushirikishwaji wa Afghanistan ni msingi wa uthabiti wa kudumu
-
Aragchi: Ushirikishwaji wa Afghanistan ni msingi wa uthabiti wa kudumu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema uthabiti wa Afghanistan unategemea kuingizwa kwake kikamilifu katika mifumo ya kisiasa na kiuchumi ya kikanda, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa majirani badala ya kutegemea nguvu za nje.
Araqchi alitoa kauli hiyo Jumapili mjini Tehran katika mkutano wa ngazi ya juu uliopewa jina “Tathmini Kuhusu Matukio ya Afghanistan”, uliowakutanisha wawakilishi maalum kutoka nchi jirani.
Akihutubia mkutano huo, Araqchi alisema uzoefu umeonyesha kuwa “mapendekezo na maamuzi kutoka nje ya eneo” hayajawahi kuleta utulivu katika mataifa yaliyokumbwa na migogoro.
Alisisitiza nafasi ya msingi ya nchi jirani katika kushughulikia changamoto za eneo, akizieleza kuwa “wahusika wa asili na wa kuaminika zaidi” katika kukabiliana na matatizo ya Afghanistan.
Araqchi pia alibainisha umuhimu wa kijiografia na kiuchumi wa Afghanistan, akisema nchi hiyo iko katika makutano ya Asia ya Kati, Asia Magharibi na Asia Kusini—nafasi inayoweza kuifanya kuwa daraja la biashara, usafirishaji wa nishati na muunganisho wa kikanda.
Waziri huyo wa mambo ya nje aliongeza kuwa uthabiti na maendeleo ya Afghanistan si suala la kibinadamu pekee, bali ni ajenda ya kimkakati kwa eneo zima, akisisitiza kuwa usalama na ustawi wa Afghanistan umefungamana moja kwa moja na maslahi ya majirani zake.
Katika chapisho lake kwenye X siku ya Jumapili, Balozi wa Pakistan nchini Iran, Muhammad Mudassir Tipu, alisisitiza dhamira ya nchi yake kuendeleza amani, maendeleo na usalama katika eneo. Pia alitaka wasiwasi wa Pakistan kuhusu ugaidi uzingatiwe.
Mkutano huo wa Tehran, ulioratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, uliwaleta pamoja maafisa kutoka Iran, Pakistan, Urusi, Uzbekistan, China, Tajikistan na Turkmenistan kwa lengo la kujadili matukio ya hivi karibuni wa Afghanistan na masuala mapana ya Asia Kusini na Asia ya Kati.
Mkutano huu wa kiwango cha juu unafuatia juhudi zilizopita—lakini ambazo hazikufanikiwa—za Qatar, Uturuki na Saudi Arabia kupatanisha Afghanistan na Pakistan, na umeonekana kama msukumo mkubwa zaidi wa kidiplomasia hadi sasa katika kutuliza mvutano unaoongezeka baina ya nchi hizo mbili.