Velayati: Iran inaiunga mkono Hizbullah ya Lebanon kwa dhati
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Kimataifa amesema kuwa, Hizbullah ni moja ya nguzo muhimu zaidi za kambi ya Muqawama na ina jukumu la kimsingi katika kukabiliana na Uzayuni. Hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, chini ya maagizo ya Kiongozi Muadhamu, itaendelea kuiunga mkono harakati hiyo ambayo iko mstari wa mbele katika Muqawama.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la IRIB, matukio ya hivi karibuni ya eneo hili na ya kimataifa yamejadiliwa katika mazungumzo ya Dk Ali Akbar Velayati na Sayyid Abdullah Safi al-Din, mwakilishi wa Hizbullah ya Lebanon hapa Tehran.
Katika mazungumzo hayo Sayyid Safi al-Din amesisitiza kuwa, Hizbullah ina nguvu zaidi hivi sasa kuliko huko nyuma na iko tayari kupigania haki za wananchi wa Lebanon kwa ushujaa na uimara zaidi na kamwe haitoweka chini silaha.
Amegusia pia jinsi Israel isivyoheshimu makubaliano ya kusitisha maigano na kusema kuwa, utawala wa Kizayuni na wafuasi wake wanapaswa kujua kwamba Hizbullah itajibu jinai za Wazayuni hao wakati wowote itakapoamua.
Mwakilishi huyo wa Hizbullah ya Lebanon hapa Tehran pia ametumia fursa hiyo kutoa shukrani zake kwa msaada kamili wanaoupata kutoka kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hasa kwa Kiongozi Muadhamu na kumkhutubu Dk Velayati akimwambia: Bw. Velayati: Umekuwa mmoja wa waungaji mkono wakuu wa Hizbullah tangu mwanzo wa kuanzishwa kwake, na umetoa mchango mkubwa na wenye ufanisi katika harakati za kambi ya Muqawama.
Kwa upande wake, Dk Ali Akbar Velayati amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuiunga mkono kwa dhati Hizbullah ambayo iko mstari wa mbele katika kambi ya Muqawama.