Balozi wa Iran UN: Marekani inahusika na machafuko ya sasa nchini Iran
-
Amir-Saeid Iravani
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameliandikia barua Baraza la Usalama la umoja huo akisema Marekani imeyageuza maandamano ya amani ya wananchi wa Iran kuwa ghasia na machafuko.
Amir-Saeid Iravani amelaani mienendo inayokiuka sheria ya Marekani na ushirikiano wake na utawala wa Kizayuni wa Israel katika kuingilia mambo ya ndani ya Iran. Amesema uingiliaji kati huo unafanyika kwa kutumia vitisho, uchochezi wa machafuko na kuvuruga amani na utulivu.
Balozi wa Iran Umoja wa Mataifa amesisitiza akisema: Tunalaani vitendo hivyo vinavyovuruga amani na ambavyo ni kinyume na Hati ya Umoja wa Mataifa.
Awali, Baraza la Usalama wa Taifa la Iran lilikuwa limetoa taarifa, -ambayo mbali na kuashiria kuwa tangu baada ya vita vya siku 12 Marekani na utawala wa kizayuni wa Israel hazijaacha kufanya chokochoko za vita na uadui dhidi ya taifa la Iran-, imesisitiza kwamba: taifa linaloheshimika la Iran litazivunja mbinu za kihujuma na kufanya uharibifu za adui kwa umoja na mshikamano wa kitaifa.
Sehemu moja ya taarifa hiyo imesema: Wakati wa vita vya siku 12 na mpaka leo utawala wa kizayuni wa Israel unaendelea kufanya dhulma dhidi ya Wairani kupitia vita mseto, na unabadilisha mbinu baadhi ya wakati. Hata hivyo, haujaacha chokochoko za vita dhidi ya taifa lisilorudi nyuma la Iran, ambapo matukio ya karibuni, japokuwa yalianza kwa kulalamikia kuvurugika kwa soko la uchumi, lakini yameibua machafuko nchini kwa uongozi na ubunifu wa adui mzayuni.
Taarifa hiyo ya Baraza la Usalama wa Taifa la Iran imeendelea kueleza: Matamshi aliyotoa Trump katika siku zilizopita yanadhihirisha kuwepo mpango wa pamoja uliofanywa na tawala hizo mbili ambao unayafanya maisha ya wananchi wa Iran yasiwe na amani.
Taarifa hiyo imemalizia kwa kusisitiza kwamba, vikosi vya usalama na vya polisi vipo kwa ajili ya kuzuia machafuko nchini; na kwa kushirikiana na wananchi vitazima kwa uthabiti njama ya kuvuruga amani ya utawala wa kizayuni na baba yake wa ubatizo, Marekani, na kuhakikisha amani inapatikana kwa ajili ya maisha ya wananchi; na katika kufikia lengo hilo, vikosi vya usalama na Idara ya Mahakama hazitaonyesha chembe ya huruma katika kuwashughuulikia watu wanaofanya hujuma na uharibifu.