Dakta Larijani: Mamluki wa Marekani na Israel wanahusika katika machafuko nchini Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135332-dakta_larijani_mamluki_wa_marekani_na_israel_wanahusika_katika_machafuko_nchini_iran
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kuwa, mikono ya Marekani na utawala wa Kizayuni katika matukio haya iko wazi na dhahiri.
(last modified 2026-01-10T12:13:06+00:00 )
Jan 10, 2026 12:11 UTC
  • Dakta Larijani: Mamluki wa Marekani na Israel wanahusika katika machafuko nchini Iran
    Dakta Larijani: Mamluki wa Marekani na Israel wanahusika katika machafuko nchini Iran

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kuwa, mikono ya Marekani na utawala wa Kizayuni katika matukio haya iko wazi na dhahiri.

Dakta Ali Larijani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema hayo alipokuwa akizungumzia machafuko ya hivi karibuni hapa nchini na kusisitiza kwamba, kuna kila Ushahidi wa kuthibitisha kwamba, Marekani na utawala ghasibu wa Israel zinahusika moja kwa moja katika kuchochea vurugu hizi.

Dakta Larijani amesema kuwa, Marekani na utawala wa Kizayuni wanajaribu kuunda msingi wa uingiliaji kati wa kigeni kwa kuchochea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Iran.

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran aliongeza: "Viongozi wa makundi ya kigaidi yenye silaha wanatafuta kuchochea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Iran."

Awali, Baraza la Usalama wa Taifa la Iran lilikuwa limetoa taarifa, -ambayo mbali na kuashiria kuwa tangu baada ya vita vya siku 12 Marekani na utawala wa kizayuni wa Israel hazijaacha kufanya chokochoko za vita na uadui dhidi ya taifa la Iran-, imesisitiza kwamba: taifa linaloheshimika la Iran litasambaratisha mbinu za kihujuma na kufanya uharibifu za adui kwa umoja na mshikamano wa kitaifa.

Sehemu moja ya taarifa hiyo imesema: Wakati wa vita vya siku 12 na mpaka leo utawala wa kizayuni wa Israel unaendelea kufanya dhulma dhidi ya Wairani kupitia vita mseto, na unabadilisha mbinu baadhi ya wakati. Hata hivyo, haujaacha chokochoko za vita dhidi ya taifa lisilorudi nyuma la Iran, ambapo matukio ya karibuni, japokuwa yalianza kwa kulalamikia kuvurugika kwa soko la uchumi, lakini yameibua machafuko nchini kwa uongozi na ubunifu wa adui mzayuni.