Qalibaf: Iran hivi sasa inapigana vita na adui katika pande 4
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135374-qalibaf_iran_hivi_sasa_inapigana_vita_na_adui_katika_pande_4
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa: Leo tunapigana vita na adui wa Kizayuni na Marekani katika pande nne za kiuchumi, kiuelewa, kijeshi na kigaidi.
(last modified 2026-01-11T10:58:17+00:00 )
Jan 11, 2026 10:58 UTC
  • Qalibaf: Iran hivi sasa inapigana vita na adui katika pande 4

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa: Leo tunapigana vita na adui wa Kizayuni na Marekani katika pande nne za kiuchumi, kiuelewa, kijeshi na kigaidi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, amesema hayo katika kikao cha wazi cha leo Jumapili na kuongeza kuwa, hivi sasa tunapigana vita na adui wa Kizayuni na Marekani katika pande 4. Amefafanua zaidi kwa kusema: Tuko katika vita vya kiuchumi, kiuelewa na vita vya kijeshi na vya kigaidi. Kumbuka kwamba vita hivi vinne vyote vinafanyika kwa wakati mmoja, kwa hivyo sote lazima tulizingatie vizuri suala hilo.

Ameongeza kuwa, vita vya kiuchumi na vita vya utambuzi na kisaikolojia vimekuwepo kwa miaka mingi ingawa katika miaka ya hivi karibuni vimekuwa vikali zaidi. Lakini vita vya (karibuni zaidi vya) moja kwa moja vya kijeshi vilianza tarehe 13 Juni 2025 kwa uvamizi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran ya Kiislamu na kwa msaada wa moja kwa moja wa kijeshi wa Marekani.

Spika Qalibaf aidha amesema: "Kilicho wazi ni kwamba adui alishindwa katika vita vya kijeshi vya siku 12 na alikubali kushindwa kiasi kwamba alifikia kubebembeleza kusitishwa mapigano, na hiyo haikuwa kitu kingine ghairi ya taufiki ya Mwenyezi Mungu na baraka Zake kwa taifa pendwa la Iran ya Kiislamu... Lazima tuseme kwamba, mafanikio hayo yalikuwa ni matunda ya ufahamu wa kihistoria, uwajibikaji na ukarimu wa taifa letu..." 

Spika wa Bunge la Iran ameongeza kuwa: Katika vita vya kiuchumi, lazima tuwe macho, hasa bunge na serikali. Suala muhimu zaidi ambalo lazima tulifuatilie ni kuhakikisha tunasonga mbele katika njia ya kudumisha utulivu wa kiuchumi; huu ni wajibu wetu sisi sote, serikali, bunge na wafanyabiashara.