Qalibaf: Taifa la Iran limemzuia adui kufikia malengo yake
-
Baqer Qalibaf
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kujitokeza tena kwa Wairani uwanjani kumebatilisha uchawi wa uadui wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran, akisisitiza: "Leo, kiini kikubwa cha Wairani milioni 90, wenye dini, mielelezo ya kisiasa na lahaja tofauti, kimesimama kidete dhidi ya adui wa kigeni, na hii ni hatua muhimu ya mwamko wa Wairani."
Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran, aliyasema hayo jana Jumatatu (Januari 12) katika mkusanyiko mkubwa wa mamilioni ya watu wa Tehran, waliokusanyika katika Uwanja wa Azadi. Maandamano kama hayo pia yalifanyika sambamba katika maeneo mengine ya Iran dhidi ya ugaidi wa Kizayuni-Kimarekani kwa ajili ya kulaani vitendo vya kigaidi vya hivi karibuni vya wafanya fujo hapa nchini. Alisema: "Tunamshukuru Mungu kwamba katika vita vya kisaikolojia vya Marekani na utawala wa Kizayuni, taifa kubwa la Iran halikumruhusu adui kufikia malengo yake na limezuia harakati zote za adui katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni, na taifa hili limesimama imara dhidi ya adui."
Qalibaf amesema kwamba baada ya miezi saba ya Vita vya Siku 12, adui hajaacha njama zake mbaya na za kijinai, na akaongeza: "Adui mhalifu anataka kuizuia Iran kuwa imara na huru. "Hii leo, suala hilo liko wazi na dhahiri kabisa. Sote tuliona kwamba rais wa Marekani ameitishia Iran hadharani na rasmi kwa sababu ameamua kuanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa kutumia visingizio mbalimbali," amesema Qalibaf.
Spika wa Bunge la Iran amesema: "Baadhi ya watu wanaojiona rasmi kuwa mamluki wa kigeni wanamkaribisha rais wa Marekani katika nchi yao na wanampendelea rais wa Marekani kuliko nchi yao. Hawa ni wale wale wanachama wa ISIS wa zamani ambao nyote mliona walichokifanya katika nchi zingine. Hawa ni wanachama wa Daesh wasio na utaifa, wanaopinga dini na mamluki wenye silaha walioanzisha vita vya kigaidi dhidi ya taifa letu."
Mohammad Baqer Qalibaf ameendelea: "Lengo lao lilikuwa kuibua hofu na wahka, na walitaka kuwatisha watu, na walianzisha mradi uleule wa machafuko ya wakati wa vita kwa njia tofauti, na walifanya vitendo vya silaha kwa mtindo wa Daesh, wakitenda uhalifu wa ukatili dhidi ya wanawake, watoto, na polisi."
Akizungumzia ukatili wa magaidi hao nchini Iran wakati wa machafuko, Qalibaf amesema: "Mmeshuhudia kwamba hawakuwa na huruma kwa mtu yeyote. Walikuja kaskazini, kusini na miji mbalimbali kulipiza kisasi kwa watu wa Iran, kuigawanya nchi na walitenda hayo kwa njia iliyosababisha hofu na woga."
Spika Qalibaf ameongeza: "Maadui zetu wamenaswa tena katika makosa ya kimahesabu, na leo wameona kwamba watoto wa Iran hawakurudi nyuma na wameilinda Iran mjini Tehran na kote nchini na wamechukua jukumu la kuimarisha usalama kwa nguvu zao zote."