Vinara wa mashambulizi ya kigaidi katika ghasia za Iran wakamatwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135494-vinara_wa_mashambulizi_ya_kigaidi_katika_ghasia_za_iran_wakamatwa
Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran imesema inaendelea kuwatambua na kuwakamata vinara wa mashambulizi ya kigaidi hivi karibuni jijini Tehran kwa ushirikiano madhubuti wa wananchi.
(last modified 2026-01-15T02:40:47+00:00 )
Jan 15, 2026 02:40 UTC
  • Vinara wa mashambulizi ya kigaidi katika ghasia za Iran wakamatwa
    Vinara wa mashambulizi ya kigaidi katika ghasia za Iran wakamatwa

Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran imesema inaendelea kuwatambua na kuwakamata vinara wa mashambulizi ya kigaidi hivi karibuni jijini Tehran kwa ushirikiano madhubuti wa wananchi.

Kwa mujibu wa wizara hiyo magaidi walilenga, maeneo ya umma na ya kidini pamoja na vikosi vya usalama na waandamanaji katika maeneo saba makuu ya Tehran wakati wa machafuko ya hivi karibuni. Magaidi hao hao pia walichoma moto misikiti miwili, wakazuia moja ya barabara kuu za jiji, na kuwaua wanachama wawili wa kikosi cha kujitolea cha wananchi maarufu kama Basij.

Kamanda mkuu wa polisi ya Iran amesema watu 297 waliokuwa wakihusika katika uharibifu wa mali ya umma wametambuliwa na kukamatwa.

Katika oparesheni za siku za karibuni dhidi ya makundi ya kigaidi, magaidi wawili waliuawa na wengine 17 kujeruhiwa.

Polisi pia wamekamata silaha mbalimbali, za moto na mapanga, pamoja na vilipuzi vilivyopatikana kwenye maficho ya wahusika.

Kesi ishirini zimefunguliwa kuhusu uhusiano wa waliokamatwa na makundi ya kigaidi yenye mafungamano na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Wakati huohuo, mazishi ya mashahidi 100 wa machafuko ya hivi karibuni yaliyoungwa mkono na mataifa ya kigeni yalifanyia Jumatano saa nane mchana kwa saa za Tehran.

Mkuu wa Shirika la Mashahidi, Ahmad Mousavi, amesema mashahidi hao, raia na maafisa wa usalama, waliuawa kwa kutumia silaha mbalimbali ikiwemo bunduki za kivita na za uwindaji, visu, mapanga na vifaa vingine vya kushambulia.

Maandamano ya amani dhidi ya hali ngumu ya kiuchumi yaligeuka kuwa ghasia wiki iliyopita, yakichochewa na matamshi ya watawala wa Marekani na Israel, huku makundi yenye silaha yakiharibu mali ya umma na kusababisha vifo na majeraha kwa raia na maafisa wa usalama.

Kwa mujibu wa taarifa kiusalama za Jamhuri ya Kiislamu, magaidi na waibua ghasia walikuwa wakipokea msaada wa kijasusi, kiutendaji, vifaa na fedha kutoka Marekani na shirika la ujasusi la Mossad la Israel.

Viongozi wa Iran wamesema kuwa kupitia ghasia hizi, mahasimu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanajaribu kufidia kushindwa kwao katika mashambulizi ya moja kwa moja ya kijeshi dhidi ya nchi hii mwezi Juni.

Serikali ya Iran imesisitiza kuwa inaendelea kuchukua hatua za kushughulikia changamoto za kiuchumi katika sekta mbalimbali, huku ikisimama imara dhidi ya jaribio lolote la kuyapotosha maandamano na kuyageuza kuwa vurugu.