Pakistan: Hatutaruhusu anga yetu itumiwe kwa ajili ya kuishambulia Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135548-pakistan_hatutaruhusu_anga_yetu_itumiwe_kwa_ajili_ya_kuishambulia_iran
Serikali ya Pakistan imetangaza kuwa, katu haitataruhusu anga yake itumiwe kwa ajili ya kuishambulia kijeshi Iran.
(last modified 2026-01-16T11:14:06+00:00 )
Jan 16, 2026 11:14 UTC
  • Pakistan: Hatutaruhusu anga yetu itumiwe kwa ajili ya kuishambulia Iran
    Pakistan: Hatutaruhusu anga yetu itumiwe kwa ajili ya kuishambulia Iran

Serikali ya Pakistan imetangaza kuwa, katu haitataruhusu anga yake itumiwe kwa ajili ya kuishambulia kijeshi Iran.

Hayo yameelezwa na Tahir Andrabi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan, ambaye amesisitiza kwamba katika sera za kimsigi za nchi hiyo, hakuna ruhusa yoyote ya kutumiwa anga yake dhidi ya nchi yoyote jirani.

Alifafanua zaidi kwa kusema: "Pakistan haijawahi kutoa ruhusa kama hiyo hapo awali wala haitaruhusu nchi yoyote katika siku zijazo kutumia anga ya Pakistan dhidi ya majirani zake."

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Pakistan imekosoa vikali msimamo wa Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu machafuko yanayochochewa na nchi za Magharibi nchini Iran.

Khawaja Muhammad Asif, Waziri wa Ulinzi wa Pakistan, ambaye amekuwa akikosoa ushirikiano wa Marekani na utawala wa Kizayuni katika mauaji ya halaiki ya Wapalestina, huku akigusia uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Iran, amemtaka Rais Trump wa nchi hiyo asimamishe kikweli mauaji ya Gaza ili kuzuia kuendelea jinai za Israel katika ukanda huo.

Waziri wa Ulinzi wa Pakistan ameongeza kuwa: "Ulimwengu mzima umeungana dhidi ya mauaji ya halaiki ya Wapalestina na uvamizi wa Israel, lakini badala ya kuingilia kati na kukomesha jinai hizo, Marekani inaendelea kuipa silaha Israel na hivyo kuchangia mauaji ya Gaza."

Wakati huo huo, wanasiasa mbalimbali wa Pakistan wamesisitiza kuwa, ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kuwa upande wa Iran katika mazingira ya sasa ambapo taifa hili la Kiislamu linaandamwa kwa njama mbalimbali.