Ayatullah Khatami: Njama za kuigawa Iran kupitia machafuko zimefeli
-
Ayatullah Khatami: Njama za kuigawa Iran kupitia machafuko zimefeli
Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa nchini Tehran amesema kuwa, njama za maadui za kuigawa Iran kupitia mamluki wao kuzusha vurugu na machafuko hapa nchini zimefeli na kugonga mwamba.
Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami, Imamu wa muda wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amesema hayo leo mbele ya hadhara ya waumini waliohudhuria ibada ya Swala ya Ijumaa na kubainisha kwamba, wajinga waliota ndoto ya kuigawa nchi lakini wamefeli katika njama zao.
Ayatullah Khatami amebainisha kwamba, wapumbavu walikaa katika moja ya nchi za eneo hili na kuandika katiba yake. Ninyi wapumbavu, mnapaswa kutambua kwamba, madhali Muirani mmoja yuko hai, basi hakuna hata kipande kidogo cha aradhi ya nchi hiyo kitakachopungua. Kwa nini hamuelewi?
Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran ameeleza kuwa, taifa la Iran lilielewa kwamba uhalifu huu na vita vya kigaidi ni mwendelezo wa vita vya siku 12 vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel na kufuatiwa na Marekani. Wachomaji moto hao hao, Daesh, waliwagombanisha watu. Washenzi hawa walifanya jambo ambalo hata Wamongolia hawangeweza kulifanya.
Ayatullah Khatami ameazungumzia pia mahudhurio ya mamilioni ya watu Januari 12 ya kuunga mkono mfumo wa Kiislamu na kulaani vitendo vya kinyama na mauaji yalayofanywa na watu waliochochewa na kununuliwa na Marekani na Israel na kusifu weledi wa ufahamu wa wananchi wa Iran. Kadhalika ameashiria hamsa ya wananchi na kujitokeza kwa wingi mjini Tehran na katika miji mingine katika shughuli ya mazishi na kuwaaga mashahidi waliouawa katika kipindi cha machafuko hapa nchini.
Aidha ametoa wito wa kuendeshwa haraka kesi za mamluki na magaidi waliohusika na mauaji ya raia na wana usalama na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria.