Marekani na Israel zimeonesha kivitendo na waziwazi chuki zao dhidi ya Iran
-
Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
Waziri wa Ulinzi nwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Tuna ushahidi madhubuti unaoonesha kwamba, Marekani, utawala wa Kizayuni na baadhi ya washirika wao waliunda kituo maalumu cha kujadili na kuchora mustakabali wa Iran baada ya kuvamiwa na magaidi.
Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh, alisema hayo jana Alkhamisi katika mkutano na kundi la wambata kijeshi wa kigeni waliopo Tehran na kuongeza kuwa: Matukio yanayotokea kwa kasi kubwa kimataifa hivi sasa yanaonesha kuwa tuko kwenye kipindi cha mpito cha kijiopolitiki na tunahama hivi sasa kutoka kwenye dunia ya kambi moja kuingia kwenye dunia ya kambi kadhaa na kuzidi kupungua nguvu za Marekani.
Amesisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapinga vikali ubeberu wa Marekani, uvamizi wa utawala wa Kizayuni na vitendo vya kigaidi na kuongeza kuwa, matukio ya eneo la Asia Magharibi yakiwemo haya yaliyotokea nchini Iran ni sehemu ya kipindi hiki cha mpito.
Amir Nasirzadeh pia amesema kuwa, kauli za kichochezi za Trump ziligeuza maandamano ya amani nchini Iran kuwa ya ghasia na vitendo vya kigaidi. Amesema: Maandamano hayo ya amani yalianza Disemba 29 2025 kwa kukusanyika baadhi ya wafanyabiashara katika soko kuu la Tehran, na Serikali ilisikiliza haraka kilio chao na hali ikaelekea kwenye utulivu. Hali hiyo ya utulivu iliendelea hadi Januari 7, 2026. Lakini kauli za kichochezi za madola ya kibeberu hasa za Donald Trump ziligeuza maandamano hayo kuwa ya ghasia na kisha ya vitendo vya kigaidi katika siku za Alkhamisi na Ijumaa za tarehe 8 na 9 Januari. Lakini tarehe 12 Januari ghasia zilipungua kwa kiasi kikubwa kutokana na makumi ya mamilioni ya wananchi wa Iran kujitokeza mitaani katika kona zote za nchi, kutangaza uungaji mkono wao wa dhati kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.