Marekani haiwezi kukwepa dhima ya jinai walizofanyiwa wananchi wa Iran
-
Gholamhossein Darzi, Balozi na Naibu wa Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa
“Gholamhossein Darzi,” Balozi na Naibu wa Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kwamba, maandamano ya amani ya wananchi u wa Iran yalitekwa nyara na magenge ya kigaidi yaliyoingizwa Iran na madola ya kigeni ili kuanzisha fujo na mauaji. Marekani haiwezi kukwepa dhima ya jinai na ukatili mkubwa waliofanyiwa wananchi wa Iran.
Naibu Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema hayo kwenye kikao cha Baraza la Usalama la umoja huo cha jana Alkhamisi na kuongeza kuwa: “Kati ya Januari 8 na 10, 2026, wananchi na serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walikumbwa na vitendo vya kigaidi na ukatili wa magenge yenye misimamo mikali kama Daesh (ISIS) kote nchini Iran.”
Mwanadiplomasia huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amesema kuwa, maandamano ya amani yaliyoanza mwishoni mwa mwezi Disemba, 2025 ya kulalamikia ugumu wa kufanya biashara na kushuka thamani sarafu ya taifa, yaliendelea kwa siku kadhaa kwa amani lakini uchochezi wa madola ya kibeberu uligeuza maandamano hayo kuwa ya ghasia, ukatili, vurugu, mauaji na uharibifu mkubwa wa mali za umma na za watu binafsi.
Miongoni mwa ukatili waliofanyiwa wananchi wa Iran na magenge hayo ya kigaidi yaliyoingizwa nchini na madola ya kibeberu yakiongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel, ni pamoja na kuchinjwa na kukatwa vichwa wananchi na maafisa wa Iran, kuchomwa moto watu wakiwa hai, kupigwa na kusababishiwa vifo maafisa wa polisi na raia wa kawaida, matumizi makubwa ya silaha za moto, na kuchomwa moto kwa makusudi magari ya wagonjwa, malori ya zimamoto, vituo vya matibabu, majengo ya makazi raia, Misikiti pamoja na kuchomwa moto Qur'ani Tukufu. Yote hayo yanaibebesha dhima Marekani, utawala wa Kizayuni na washirika wao, na hawawezi kukwepa dhima ya jinai hizo.