Vikosi vya usalama Iran vyanasa silaha 60,000 zilizokuwa zikielekea Tehran
-
Moto uliowashwa na magaidi wanaopata himaya ya Marekani na Israel mitaani Tehran
Vikosi vya usalama vya Iran vinasema vimekamata silaha 60,000 zilizokuwa zikielekezwa Tehran, na kuvunja mtandao wa kigaidi uliopata mafunzo kutoka shirika la kijasusi la Israel, Mossad. Magaidi hao walihusika katika machafuko ya hivi karibuni ambapo waliua raia na maafisa wa usalama baada ya maandamano yaliyokuwa ya amani kugeuzwa na madola ya kigeni kuwa vurugu.
Kamandi ya Utekelezaji Sheria ya Iran (FARAJA) ilitangaza kwamba “silaha elfu sitini zimegunduliwa zikwa mikononi mwa wahusika wa vurugu huko Bushehr." Kamandi hiyo imeongeza kuwa silaha hizo zilikuwa zikipelekwa Tehran.
Kulingana na taarifa hiyo, magaidi wawili pia walikamatwa katika operesheni hiyo.
Wakati huohuo, vikosi vya usalama Iran pia vimeweza kubaini na kuwakamata wanachama wa “kikundi hatari cha kigaidi chenye silaha” ambacho kilikuwa kimetumwa kuua raia.
Kulingana na shirika la habari la Tasnim, mtandao huo ulipatiwa mafunzo na Mossad katika mbinu za juu za mapigano ya mijini, na ulipewa jukumu la kutumia machafuko yaliyotokea kusababisha vifo, “baada ya kutekeleza uhalifu mwingi wa kigaidi”.
Baada ya kupokea aina mbalimbali za silaha na vifaa vya mapigano ya mijini kutoka kwa vinara walioteuliwa, kundi hilo lilijipenyeza katika mitaa ya mji mkuu na kufyatua risasi kwa raia, na kusababisha mamia ya watu kuuawa na kujeruhiwa, kwa mujibu wa taarifa hiyo.
Picha zilizopatikana zikionesha harakati za kundi hilo la kigaidi zinaonyesha usambazaji wa silaha za aina tofauti, ikiwemo bunduki za AK‑47 na ‘shotgun’, pamoja na vifaa vya mawasiliano kama simu za satelaiti, ambavyo vilitumiwa na magaidi hao waliopatiwa mafunzo kuua mamia ya watu.
Wanachama wa mtandao huo pia walishambulia makao ya kijeshi na ya polisi, wakaiba silaha na kuzisambaza kwa lengo la kuchochea mapigano ya mijini na kuongeza idadi ya vifo.
Wakati wa operesheni hiyo, “idadi kubwa ya aina mbalimbali za silaha, risasi na vifaa vya satelaiti viligunduliwa na kukamatwa,” iliongeza taarifa hiyo.
Yale yaliyokuwa maandamano ya amani mwishoni mwa mwezi uliopita yaligeuka taratibu kuwa vurugu, huku wahuni wakivamia miji mbalimbali nchini, wakiwaua askari wa usalama na raia, na kushambulia miundombinu ya umma.
Maafisa wa Iran wamehusisha vurugu hizo na matendo ya kigaidi na Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Wakuu wa Marekani na shirika la ujasusi la Israel, Mossad, wamekiri kuhusika moja kwa moja katika matukio hayo, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani wa zamani, Mike Pompeo, akituma ujumbe kwenye mtandao wa X akisema: “Heri ya Mwaka Mpya kwa kila Muirani aliye mitaani. Pia, kwa kila wakala wa Mossad anayetembea pamoja nao.”
Katika chapisho la mitandaoni kwa lugha ya Kifarsi, Mossad iliwahamasisha wahusika wa vurugu “Kutoka kwa pamoja mitaani. Wakati umefika,” ikiongeza kuwa mawakala wa Mossad wako pamoja nao “si tu kwa mbali na kwa maneno. Tuko [pamoja nao] uwanjani.”