"Jeshi la Iran litakata 'mkono wowote wa chokochoko' dhidi ya Kiongozi Muadhamu"
Afisa wa ngazi ya juu wa Jeshi la Iran amepuuzilia mbali vitisho vya maneno vya hivi karibuni vya Rais wa Marekani Donald Trump, akionya kwamba, hatua yoyote ya uadui itakayoelekezwa kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei itakabiliwa na kisasi kikubwa cha kijeshi.
Jenerali Abolfazl Shekarchi, Msemaji wa Vikosi vya Jeshi la Iran amesema hayo katika mkutano uliofanyika jana Jumanne hapa mjini Tehran na kusisitiza kuwa: "Hatuzingatii kwa umuhimu mkubwa kelele za Trump."
Jenerali Shekarchi amepinga vitisho hivyo kutoka kwa Trump, ambaye hivi karibuni alibwabwaja na kudai kuwa uongozi wa Iran lazima ubadilike, kama sehemu ya kampeni pana ya vita vya kisaikolojia.
"Trump anajua kwamba ikiwa mkono wa uchokozi utaelekezwa kwa Kiongozi wetu, hatutaukata tu mkono huo, na hii si kaulimbiu tu, lakini tutawasha moto kwenye ulimwengu wao na kuwaacha bila kuwa na pahali salama katika eneo," Jenerali Shekarchi amesisitiza.
Kamanda huyo wa Jeshi la Iran ameeleza bayana kuwa, "Maadui wanafahamu hili, lakini wanaendelea na vita vyao vya utambuzi."
Amebainisha kuwa, maadui wanajua kwamba, iwapo shibri yoyote ya ardhi yetu itahujumiwa, tutaliondoa tishio hilo kabla halijapanuka, akirejelea mfano wa vita vya siku 12 vya Juni, 2025 kama mfano wa kihistoria wa uwezo huo.
Haya yanajiri siku chache baada ya Rais Masoud Pezeshkian wa Iran kuonya pia kwamba, shambulio lolote dhidi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu litakuwa "vita kamili" na taifa la Iran.