Iran yamuita balozi wa Ujerumani kulalamikia 'uadui' wa Berlin
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imemuita balozi wa Ujerumani hapa mjini Tehran kulalamikia misimamo na hatua za hivi karibuni za uadui zilizochukuliwa na mamlaka za Ujerumani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Axel Dittmann aliitwa na Alireza Yousefi, Mkurugenzi Mkuu wa Ulaya Magharibi katika wizara hiyo, jana Jumanne, na kuarifiwa rasmi kuhusu malalamiko makali ya Jamhuri ya Kiislamu.
Wizara hiyo imebainisha kuwa, sababu ya kuitwa balozi huyo ni "vitendo dhidi ya Iran nchini Ujerumani na misimamo ya uharibifu iliyochukuliwa na maafisa wa Ujerumani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kinyume na sheria za kimataifa."
Wakati wa mkutano huo, Yousefi amelaani misimamo ya uadui ya Ujerumani "hasa nchi hiyo ya Ulaya kuwa mwenyeji wa makundi ya vurugu na ya kigaidi" ambayo ni maadui za Tehran.
Amesisitiza kwamba, misimamo na hatua kama hizo zinapingana na kanuni za msingi za sheria za kimataifa na Hati ya Umoja wa Mataifa.
Balozi wa Ujerumani hapa nchini ameahidi kuwasilisha malalamiko ya Tehran kwa mamlaka husika za Berlin.
Mamlaka za Ujerumani zimekuwa zikichukua misimamo ya uadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, sambamba na Marekani kuendelea kutishia kuishambulia kijeshi Iran.