Pezeshkian: Iran haitasalimu amri mbele ya madola ya kibeberu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137418-pezeshkian_iran_haitasalimu_amri_mbele_ya_madola_ya_kibeberu
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema taifa hili halitasalimu amri kamwe mbele ya madola ya kibeberu, huku akiitaka jamii ya kimataifa kulaani uvamizi wa Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
(last modified 2026-03-17T09:34:39+00:00 )
Mar 17, 2026 09:34 UTC
  • Pezeshkian: Iran haitasalimu amri mbele ya madola ya kibeberu

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema taifa hili halitasalimu amri kamwe mbele ya madola ya kibeberu, huku akiitaka jamii ya kimataifa kulaani uvamizi wa Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Rais Pezeshkian amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X Jumatatu, ambapo ameiasa jamii ya kimataifa kuzilazimisha tawala vamizi za Marekani na Israel kuheshimu sheria ya kimataifa.

Rais wa Iran ameashiria mazungumzo yake ya simu ya hivi karibuni na mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron na kubainisha kuwa, "Katika mazungumzo ya simu na Rais wa Ufaransa, nilisisitiza kuwa Iran haikuanzisha vita hivi."

Dakta Pezeshkian ameeleza bayana kuwa, kujilinda dhidi ya uvamizi ni haki ya asili na isiyopingika ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaifahamu vyema.

Amesema hatua ya Marekani ya kutumia kambi zake za kijeshi katika eneo hili la Asia Magharibi kuishambulia Iran inalenga kuvuruga uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu na majirani zake.

"Amani na utulivu haviwezi kushuhudiwa katika eneo kwa kupuuzwa uvamizi na hujuma za kichokozi za Marekani na Israel dhidi ya Iran," amebainisha Rais wa Iran.

Pezeshkian amesisitiza kuwa, kamwe taifa la Iran halitasalimu amri mkabala wa madola ya kibeberu, huku akiitaka jamii ya kimataifa kulaani chokochoko za Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Ameongeza kuwa, kuzungumza kuhusu usitishaji vita hakuna maana yoyote mpaka pale maadui wavamizi watakapotiwa adabu wasithubutu tena kuishambulia nchi hii.