Iran yasema misimamo ya Marekani “inayobadilika na kinzani” imekwamisha mazungumzo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i138972-iran_yasema_misimamo_ya_marekani_inayobadilika_na_kinzani_imekwamisha_mazungumzo
Iran imesema mazungumzo yanayoendelea na Marekani bado yamekwama hasa kutokana na misimamo ya Washington inayobadilika mara kwa mara na yenye kauli zinazokinzana. Aidha Marekani inaendelea “kubadilisha vigezo vya mazungumzo.” Hata hivyo, ubadilishanaji wa ujumbe kati ya pande hizo mbili unaendelea kupitia wapatanishi kutoka Pakistan.
(last modified 2026-06-08T03:23:36+00:00 )
Jun 08, 2026 03:21 UTC
  •  Esmaeil Baghaei
    Esmaeil Baghaei

Iran imesema mazungumzo yanayoendelea na Marekani bado yamekwama hasa kutokana na misimamo ya Washington inayobadilika mara kwa mara na yenye kauli zinazokinzana. Aidha Marekani inaendelea “kubadilisha vigezo vya mazungumzo.” Hata hivyo, ubadilishanaji wa ujumbe kati ya pande hizo mbili unaendelea kupitia wapatanishi kutoka Pakistan.

Katika mahojiano maalum na mwandishi mwandamizi wa masuala ya kimataifa wa CNN, Frederik Pleitgen, yaliyofanyika Tehran Jumapili, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, alithibitisha kuendelea majadiliano kwa njia ya maandishi kati ya Tehran na Washington kupitia wapatanishi wa Pakistan.

Amesema: “Tatizo kuu la kufanya mazungumzo na utawala uliopo Marekani ni kwamba unakumbana na misimamo mingi inayobadilika, kubadilishwa kwa masharti ya mazungumzo na kauli tofauti na zinazokinzana kutoka kwa maafisa mbalimbali, jambo linalofanya mchakato mzima kuwa mgumu sana.”

Baghaei ameongeza kuwa bado kuna masuala kadhaa ambayo hayajapatiwa suluhu katika mazungumzo ya kufikia hati ya makubaliano ya awali (MOU). Amesisitiza tena umuhimu wa Marekani kutambua haki za Iran, ikiwemo haki ya kuendeleza urutubishaji wa madini ya nyuklia ya urani kwa malengo ya amani chini ya Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT).

Msemaji huyo pia ameitaka Marekani iachie bila masharti mabilioni ya dola ya mali za Iran zinazozuiliwa katika benki za kigeni, akipinga wazo kwamba hatua hiyo inaweza kuonekana kama aina ya upendeleo au makubaliano maalum.

Kwa miongo kadhaa, Marekani imekuwa ikishikilia mabilioni ya dola ya mali halali ya Iran,  ikiwa ni pamoja na mapato ya mafuta, akiba za benki kuu na mali za kibiashara , ambazo zimechukuliwa kupitia amri za kiutendaji zisizo halali na kudumishwa kwa shinikizo la kisiasa.

Siku chache baada ya kusitishwa kwa mapigano kufuatia mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yaliyoanza tarehe 28 Februari, suala la mali zilizogandishwa za Iran limeibuka kuwa kipimo muhimu cha nia ya dhati ya Marekani katika mazungumzo.

Msemaji huyo wa Iran pia amesema kuwa Marekani imekuwa ikikiuka usitishaji mapigano ulioanza mwezi Aprili kwa kushambulia meli za kibiashara za Iran.

Amesema hali ya sasa katika eneo ni “tete sana na hatari,” akilaumu mtazamo wa “kutojali na wa hatari” wa Marekani kuhusu eneo na makubaliano ya kusitisha mapigano.

Baghaei ameonya kuwa Vikosi vya Ulinzi vya Iran “viko imara na vimeazimia kujibu mashambulizi yoyote kwa nguvu zote.”