Sisitizo la Iran la kuendelea kuiunga mkono Syria katika kupambana na ugaidi
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaitakidi kuwa kulindwa umoja, mshikamano na ardhi yote ya nchi zote za Mashariki ya Kati ikiwemo Syria ni suala la msingi. Aidha ni jukumu lake kutoa msaada katika kupambana na ugaidi na kurejesha amani na usalama nchini Syria na kwamba kubadilishwa mipaka ya nchi hiyo hakuwezi kamwe kuwa na maslahi kwa eneo hili.
Hayo yameelezwa na Rais Hassan Rouhani katika mazungumzo na Bi Hadiya Khalaf Abbas, Spika wa Bunge la Syria. Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika jana hapa mjini Tehran, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema: "Leo wananchi wa Syria wamehimilishwa vita vya kidhalimu na makundi ya kigaidi ambayo hayaheshimu misingi yoyote ya kiakhlaqi na kiutu; na muqawama na kusimama imara wananchi hao katika mazingira magumu ya kukabiliana na ugaidi kwa muda wa miaka mitano sasa ni jambo linalostahili pongezi."
Huku akiashiria kwamba ni jambo la kusikitisha kuona leo hii nchi nyingi za Kiislamu katika eneo zimezongwa na njama zinazofanywa na maadui, huku wananchi wa mataifa mbalimbali ikiwemo Yemen, Iraq, Syria, Libya na Afghanistan wakikabiliwa na hali ngumu na matatizo makubwa, Dakta Rouhani alisisitiza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko imara katika misimamo yake; na kwa kuzingatia kuwa ugaidi ni janga kubwa kwa eneo na dunia nzima kwa jumla inaitakidi kwamba ni lazima wananchi wa Syria wasaidiwe ili waweze kuutimua ugaidi hadi nje ya nchi yao; na nchi nyinginezo pia hazina njia nyingine ya kupambana na ugaidi ghairi ya hiyo."
Hivi karibuni, alipohutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alizungumzia pia suala hili; na huku akiashiria vizuizi vinavyowekwa ili usipatikane ufumbuzi wa kimantiki wa kutatua mgogoro wa miaka mitano nchini Syria, Dakta Rouhani alirudia tena kauli yake aliyotoa alipohutubia rasmi mara ya pili Baraza Kuu la umoja huo aliposema: "Wakati majenerali wamefunguliwa njia kuingia katika eneo, msitarajie wanadiplomasia watatoka kwenda kuwalaki". Hii ni indhari ambayo nchi za Magharibi hazikuizingatia; na leo hii tunashuhudia migogoro ikiendelea huku mgogoro wa Syria ukiwa ndio mgogoro mkubwa zaidi katika eneo hili.
Suala la Syria hivi sasa limekuwa ndicho kipaumbele cha kwanza cha jitihada zinazofanywa kieneo na kimataifa. Hivi karibuni Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliijadili tena kadhia hiyo kwa matumaini ya kuweza kuondoa vizuizi vinavyokwamisha kuendelea usitishaji vita nchini humo, lakini mitazamo ya Marekani juu ya suala hili imekuwa ni ya upande mmoja na ya kuyaunga mkono makundi ya kigaidi kiasi ambacho jitihada zote zilizofanywa hadi sasa zimeshindwa kuwa na tija.
Kilicho na umuhimu katika mazingira hasasi na nyeti ya hivi sasa ni kuwafikishia misaada wananchi wa Syria na kuwaondolea mzingiro waliowekewa na magaidi. Kwa mtazamo huo, kupambana na makundi yote ya kigaidi, liwe la Daesh au la An-Nusrah sambamba na kuwafikishia misaada wananchi ni jambo la lazima.
Katika medani za mapambano, hivi sasa tunashuhudia ushindi mkubwa linaopata jeshi la Syria. Duru za habari zimeripoti kuwa shambulio la ardhini lililofanywa na vikosi vya jeshi la Syria katika mji wa Aleppo, ndilo kubwa zaidi kuwahi kufanywa tangu ilipoanza duru mpya ya mashambulio ya kuukomboa mji huo. Bila ya shaka kungali kuna safari ndefu hadi ushindi kamili. La kufanya ni kusubiri kuona, kusonga mbele kwa jeshi la Syria na msimamo wa wazi wa Syria na Russia wa kupinga uanzishaji eneo la marufuku ya kuruka ndege katika anga ya Syria ambako kuna nafasi muhimu zaidi katika kupambana na makundi ya kigaidi, vitakabiliwa na jibu na radiamali gani ya Marekani.
Ni wazi kuwa serikali halali ya Syria ndio marejeo pekee yenye uwezo wa kutoa maamuzi kuhusu mustakabali wa nchi hiyo. Na bila ya shaka mazungumzo baina ya serikali na wapinzani wenye msimamo wa kutetea uhuru, kujitawala na matakwa ya taifa la Syria kwa ajili ya kupata njia ya ufumbuzi wa kisiasa na makubaliano kamili yatakayojumuisha matakwa na ushirikishaji wa makabila, dini na madhehebu zote nchini Syria ndilo chaguo mwafaka litakalosaidia kutatua mgogoro wa nchi hiyo.
Ni wazi kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuisaidia Syria katika kupambana na ugaidi na kurejesha amani na usalama nchini humo na katika eneo kwa jumla.
Nayo Marekani, kama ina nia ya kweli ya kuwasaidia wananchi wa Syria inapaswa ifanye jithada za dhati za kukomesha ugaidi ambao ni hatari kwa eneo hili na ulimwengu mzima.../