Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman aonana na Rais Rouhani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i1675-waziri_wa_mambo_ya_nje_wa_oman_aonana_na_rais_rouhani
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kwamba, kuna wajibu wa kuimarishwa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara wa Iran na Oman na kuufikisha kwenye daraja ya uhusiano wa kisiasa wa pande hizo mbili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 21, 2016 12:32 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman aonana na Rais Rouhani

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kwamba, kuna wajibu wa kuimarishwa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara wa Iran na Oman na kuufikisha kwenye daraja ya uhusiano wa kisiasa wa pande hizo mbili.

Rais Rouhani amesema hayo leo wakati alipoonana na Bw. Yusuf bin Alawi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, uhusiano wa nchi hizi mbili ni wa kiistratijia. Amesema, kuna haja ya kuimarishwa uhusiano wa kiuchumi na kibiashara wa nchi mbili kwa kiwango cha juu sana.

Amesema, uhusiano wa Tehran na Muscat ni kigezo cha uhusiano bora katika eneo hili, na kwamba Tehran ina hamu ya kuona uhusiano wake wa kibiashara na kiuchumi na Muscat unapanda na kufikia daraja ya uhusiano wa kisiasa wa pande mbili.

Aidha ameishukuru Oman kwa misimamo yake mizuri katika kadhia ya nyuklia ya Iran na kusema, misimamo hiyo ya Oman ilichukuliwa kwa nia ya kuimarisha usalama kwenye eneo hili.

Kwa upande wake, Bw. Yusuf bin Alawi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman amesema kuwa, nchi yake inasisitizia suala la kuimarisha uhusiano wake na Iran katika nyuga zote na ndio maana limewawekea mazingira mazuri sana wafanyabiashara wa Kiiran ili wafanye biashara kwa uhuru kamili nchini Oman.