IAEA yasisitizia, Iran imeheshimu makubaliano ya JCPOA
Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) umesisitiza tena katika ripoti yake mpya kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza na kuheshimu makubaliano ya nyuklia maarufu kama JCPOA kwa kifupi.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, Yukia Amano amesisitiza katika ripoti yake mpya kuhusu makubaliano ya miradi ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 kwamba, Tehran imetekeleza makubaliano hayo.
Baada ya kutolewa ripoti hiyo ya msimu, mwakilishi wa Iran katika Wakala wa IAEA, Reza Najafi amesema kuwa, ripoti mpya ya Yukia Amano imethibitisha tena kwamba, Iran imetekeleza kikamilifu makubaliano ya JCPOA.
Najafi ameongeza kuwa, ripoti hiyo imeonesha tena kwamba, miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran inafanyika kwa mujibu wa sheria za kimataifa na makubaliano ya JCPOA katika sekta sote za kurutubisha madini ya urani, uhakiki na utafiti, ujenzi mpya wa kinu cha nyuklia cha Arak na uzalishaji wa maji mazito.