Zarif: Ubeberu wa nchi za Magharibi duniani umepitwa na wakati
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i21241-zarif_ubeberu_wa_nchi_za_magharibi_duniani_umepitwa_na_wakati
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, zama za uistikbari na ubeberu wa madola makubwa ya Magharibi zimepita na kwamba enzi hizo hazina nafasi katika dunia ya sasa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 12, 2016 02:39 UTC
  • Zarif: Ubeberu wa nchi za Magharibi duniani umepitwa na wakati

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, zama za uistikbari na ubeberu wa madola makubwa ya Magharibi zimepita na kwamba enzi hizo hazina nafasi katika dunia ya sasa.

Mohammad Javad Zarif aliyasema hayo jana Jumapili katika Kongamano la Kimatifa la Usalama wa eneo la Magharibi mwa Asia hapa mjinin Tehran na kuongeza kuwa, Marekani imetumia mabilioni ya dola kuzivamia na kuzishambulia baadhi ya nchi kwa shabaha ya kutaka kuonekana 'dola kubwa' lakini hatua zake hizo hazijazaa matunda.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, eneo la Magharibi mwa Asia karibuni hivi litakuwa na nafasi muhimu sana katika mfumo na siasa za kimataifa.

Mkutano wa Usalama mjini Tehran

Mohammad Javad Zarif amesisitiza kuwa, usalama wa eneo hili unahitaji ushirikiano wa nchi za eneo na wala sio uingiliaji wa nchi ajinabi.

Lengo la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran la kubuni mkutano wa kiusalama wa Tehran ni kufanyika juhudi za kunufaika na kiigizo kilichofanikiwa cha ushirikiano wa makubaliano ya nyuklia katika kuleta nidhamu na kuweka mikakati mipya ya kiusalama katika eneo la magharibi mwa Asia.

Wataalamu na wanafikra katika masuala ya usalama wa eneo hili kutoka nchi mbalimbali wameshiriki katika mkutano huo lengo hasa likiwa ni kuwa na ufahamu kuhusiana na eneo hili na hivyo kuweka mikakati ya kudumisha amani na usalama wa wote. Mkutano huo ulifunguliwa kwa hotuba ya Dakta Ali Larijani, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye alisisitiza kuwa umuhimu wa kuweko mazungumzo, hali ya kuaminiana na ushirikiano wa pamoja wa nchi za eneo la magharibi mwa Asia ni kupatikana usalama na maendeleo ya wote.