Iran, Luxemberg zasisitizia haja ya kuheshimiwa makubaliano ya nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i25136-iran_luxemberg_zasisitizia_haja_ya_kuheshimiwa_makubaliano_ya_nyuklia
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Luxemberg zimesisitizia umuhimu wa kuheshimiwa na kutekelezwa kikamilifu makubaliano ya nyuklia ya Vienna.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 14, 2017 10:46 UTC
  • Iran, Luxemberg zasisitizia haja ya kuheshimiwa makubaliano ya nyuklia

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Luxemberg zimesisitizia umuhimu wa kuheshimiwa na kutekelezwa kikamilifu makubaliano ya nyuklia ya Vienna.

Rais Hassan Rouhani wa Iran na Jean Asselborn, Waziri wa Mambo ya Nje wa Luxemberg ambaye yuko safarini hapa nchini wamesema leo Jumanne hapa mjini Tehran kuwa, pande zote husika katika makubaliano hayo ya nyuklia ya Iran zinapaswa kujitolea kwa dhati kutekeleza mapatano hayo

Dakta Rouhani amesisitiza kuwa, makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 ni kwa maslahi na manufaa ya pande zote zilizosaini mapatano hayo huko Vienna Julai mwaka 2015 na kubainisha kwamba, Iran itaendelea kuheshimu na kutekeleza wajibu wake katika makubaliano hayo madhali upande wa pili hautayakiuka.

Rais Rouhani na Waziri wa Mambo ya Nje wa Luxemberg

Akiashiria kuwa nchi yake sawa na nchi nyingine za Umoja wa Ulaya zinaunga mkono kikamilifu utekelezwaji wa makubaliano hayo, Jean Asselborn, Waziri wa Mambo ya Nje wa Luxemberg amesema kuwa, amani haipatikani iwapo mapatano yoyote ya pande mbili au pande tatu yatakiukwa na kutoheshimiwa na upande mmoja. 

Mbali na kadhia hiyo ya makubaliano ya nyuklia ya Iran, Rais wa Iran na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Luxemberg wamesisitiza kuwa, ushirikiano kati ya Tehran na EU unaweza kuwa na taathira chanya katika vita dhidi ya ugaidi na misimamo ya kuchupa mipaka katika eneo hili la Mashariki ya Kati.