Zarif: Saudi Arabia ingali inavuruga uthabiti Mashariki ya Kati
Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Mohammad Javad Zarif amesema Saudi Arabia haijabadilisha sera zake za uhasama na ingali inavuruga uthabiti wa Mashariki ya Kati.
Katika mahojiano na shirika la habari la ISNA Jumapili, Zarif amesema Saudi Arabia ilikuwa imeweka matumaini yake katika mtazamo kuhusu Iran uliokuwepo katika uga wa kimataifa kabla ya mapatano ya kihistoria ya nyuklia ya Julai 2015 kati ya Iran na madola sita makubwa duniani ya kundi la 5+1. Amesema inasikitisha kuona baadhi ya nchi za eneo zilikuwa zinafurahia kuona Iran ikishinikizwa na kuwekewa vikwazo. Hata hivyo amesema baada ya mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA), madola hayo hasimu ya kieneo yamekuwa yakijaribu kila yawezalo kuona Iran inashinikizwa na kuwekewa vikwazo tena.
Itakumbukwa kuwa mapatano hayo ya nyuklia yalifikiwa Julai 14 mwaka 2015 baina ya Iran na wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaani China, Russia, Uingereza, Ufaransa na Marekani pamoja na Ujerumani na kuanza kutekelezwa Januari mwaka 2016. Kwa mujibu wa mapatano hayo, Iran iliaahidi kusitisha baadhi ya shughuli zake za nyuklia kwa malengo ya amani mkabala wa kuondolewa vikwazo vya kidhalimu.

Zarif amesema baadhi ya nchi zinazopakana na Iran ambazo zinashirikiana na maadui wa nchi hii hivi karibuni zitafikia natija kuwa, sera za kuishinikiza Tehran hazina natija yoyote na kwamba mazungumzo na Iran ndio njia pekee ya kutatua matatizo ya eneo. Aidha amesema baadhi ya nchi jirani ambazo zinaunga mkono magaidi sasa zimeanza kupoteza ushawishi kutokana na sera zao potovu. Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran amesema hakuna haja ya kuwepo mpatanishi baina ya Tehran na Riyadh lakini akasema Iran haipingi jitihada za baadhi ya nchi kujaribu kurejesha uhusiano baina ya pande hizi mbili.