Trump na vitisho dhidi ya Iran kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu
Ayatullah Sayyed Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu jana Jumapili alikutana mjini Tehran na familia za mashahidi walinzi wa Haram Takatifu na vikosi vya usalama vinavyolinda mipaka ya nchi na kusisitiza umuhimu wa mashahidi katika uhai wa Iran.
Katika hotuba yake Kiongozi Muadhamu aliashiria vitisho vya hivi karibuni vya wakuu wa Marekani na kuvitaja kuwa vya kijuba na kusema: "Matamshi ya kijuba ya rais wa Marekani si jambo jipya. Hii ni kwa sababu tokea mwanzo wake, Mfumo wa Kiislamu umekuwa ukikabiliwa na njama mbali mbali lakini wanaolitakia mabaya taifa la Iran hawawezi kufanya lolote."
Kiongozi Muadhamu aliashiria pia matamshi ya wakuu wa Marekani ambao katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakisema wanatekeleza jitihada za kutaka kuubadilisha mfumo wa Kiislamu Iran na kuongeza kuwa: "katika kipindi cha miaka 38 iliyopita, wamekuwa wakipanga njama za kuubadilisha Mfumo wa Kiislamu lakini njama zao hizo zimekuwa zikigonga mwamba na hali itaendelea kuwa hivyo katika siku za usoni."
Iwapo tutaangazia historia ya uhasama wa Marekani dhidi ya Iran katika nusu karne iliyopita, tutaona kuwa, daima Marekani imekuwa ni tishio kwa Iran.
Vitisho hivyo viko katika miundo mbali mbali ikiwa ni pamoja na vita laini ambavyo vingali vinaendelea na hiyo ni ishara kuwa Marekani inalenga kutumia kila njia iwezekanayo kuudhuru Mfumo wa Kiislamu.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi sasa ni nchi iliyopata umaarufu duniani kama nchi yenye kusimama kidete katika kukabiliana na Marekani na madola ya kibeberu duniani. Mapambano hayo ya kudumu ya Iran yamethibitisha kuwa taifa na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unamfahamu vizuri adui na utambulisho wake.
Hawa ni maadui ambao wakati mmoja walimuunga mkono Saddam katika vita vyake dhidi ya Iran na hivyo kueneza vita Mashariki ya Kati. Hawa ni maaadui ambao leo wameibua magaidi na sasa wanatumia kisingizio cha vita dhidi ya ugaidi kubadilisha ramani ya kisiasa Asia Magharibi au Mashariki ya Kati.
Tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ulitoa pigo kwa Marekani na hivi sasa wakuu wa Marekani, wawe ni Wademocrat au Warepublican, wamekuwa wakitumia lugha ya vitisho dhidi ya Iran.
Kufuatia ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa rais Marekani mwaka 2016, kuliibuka maswali mengi kuhusu mabadiliko tarajiwa katika sera za Washington ikiwa ni pamoja na uhasama wa nchi hiyo dhidi ya Iran. Wengi walihoji iwapo kutakuwa na tofauti baina ya Trump na marais waliomtangulia kama vile, Reagan, Bush, Clinton au Obama, na iwapo kungekuwa na tofauti katika uhasama wa Marekani dhidi ya Iran.
Marie-Cécile Naves ni Mfaransa mchambuzi wa masuala ya Marekani na ktika tathmini yake kumhusu Trump anasema: "Donald Trump anataka kuwepo makabiliano na Iran ili kwa njia hiyo abadilishe mlingano wa Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) na hatimaye kuibua mabadiliko katika jiografia ya kisiasa. Analenga kuhakikisha kuwa mabadiliko kama hayo yanakuwa kwa malengo ya kiuchumi. Muelekeo huo unaenda sambamba na shakhsia ya Trump."
Ukweli ni kuwa, katika hali ya hivi sasa katika eneo, kuibuka watu kama Trump ni mirathi ya watawala waliotangulia Marekani. Tusisahau kuwa, hakuna tafauti kubwa baina ya utambulisho wa tabia za Trump na marais waliomtangulia Marekani.
Kilicho tofauti ni kuwa, Trump hana uzoefu ikilinganishwa na wenzake waliomtangulia wala busara ya kisiasa hata kidogo.
Lakini kabla ya Trump na wapambe wake kudiriki ukweli wa mambo Marekani na duniani, yumkini matukio yasiyotabirika yakatokea na hilo kumalizika kwa madhara ya Marekani na nchi zingine duniani.
Wakuu wa Marekani wawe waliotangulia au waliopo hivi sasa, wamefanya kila wanaloweza kuidhuru na kutoa pigo kwa Iran. Kwa msingi huo Trump anapaswa kufahamu kuwa, kila atakayejaribu kuidhuru Iran hakuna shaka kuwa ndiye atakayepata hasara.
Kama alivyosisitiza Kiongozi Muadhamu: "Wote, wawe maadui au marafiki wenye ikhlasi wafahamu kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko imara na inasimama kwa uwezo kamili na wala maadui hawawezi kuidhuru Iran bali ni taifa la Iran ndilo litakalotoa pigo kwa adui."