Jul 29, 2017 13:48 UTC
  • Ayatullah Araki: Hujuma dhidi ya Msikiti wa al-Aqswa hazitaachwa bila majibu

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amesema kuwa, mashambulio ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina na Msikiti wa al-Aqswa ni hujuma dhidi ya ubinadamu na kwamba, mashambulio hayo hayatabikia hivi hivi bila majibu.

Ayatullah Sheikh Mohsen Araki amesema kuwa, Israel ni utawala bandia usio na utambulisho na kuongeza kuwa, mashambulio dhidi ya Waislamu wa Palestina yanayofanywa na utawala haramu wa Israel ni mwendelezo wa hatua za chuki na uhasama za Wazayuni.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amesema kuwa, hujuma hizo za Wazayuni zimekabiliwa na radiamali mbalimbali katika kila pembe ya dunia na hata barani Ulaya na Marekani. 

Askari wa utawala haramu wa Israel wakiuvamia Msikiti wa al-Aqswa

Ayatullah Araki amesema kuwa, daima Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikiunga mkono watu wanyonge na madhulumu duniani na itaendelea kufanya hivyo na kwamba, mzingiro dhidi ya Qatar, Yemen na Iran utafikia tamati hivi karibuni na kitu pekee kitakachobakia ni chuki na uhasama wa wananchi dhidi ya mataifa ya vibaraka katika Mashariki ya Kati na ulimwenguni kwa ujumla.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu ameashiria siasa za kindumakuwili za Marekani kuhusiana na kadhia ya makundi ya kigaidi katika Mashariki ya Kati na kusema kuwa, kuenea ugaidi katika maeneo mbalimbali duniani ni matokeo ya siasa za Washington katika uga wa kimataifa hususan eneo la Mashariki ya Kati.

 

Tags