Ayatullah Larijani: Wamarekani hawajajifunza kutokana na mapambano ya Wairani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i32518-ayatullah_larijani_wamarekani_hawajajifunza_kutokana_na_mapambano_ya_wairani
Mkuu wa Idara ya Mahakama nchini Iran amesema kuwa mfumo wa Kiislamu wa Iran kwa sasa ni imara na madhubuti zaidi kuliko wakati wowote mwingine na kuongeza kuwa: Wamarekani hawajapata ibra na mafunzo kutokana na muqawama na kusimama kidete kwa wananchi wa Iran katika kipindi chote cha miaka iliyopita.
(last modified 2026-08-17T09:53:57+00:00 )
Jul 31, 2017 10:42 UTC
  • Ayatullah Larijani: Wamarekani hawajajifunza kutokana na mapambano ya Wairani

Mkuu wa Idara ya Mahakama nchini Iran amesema kuwa mfumo wa Kiislamu wa Iran kwa sasa ni imara na madhubuti zaidi kuliko wakati wowote mwingine na kuongeza kuwa: Wamarekani hawajapata ibra na mafunzo kutokana na muqawama na kusimama kidete kwa wananchi wa Iran katika kipindi chote cha miaka iliyopita.

Ayatullah Sadiq Amoli Larijani ambaye leo alikuwa akihutubia kikao cha maafisa wa ngazi za juu wa Idara ya Mahakama mjini Tehran amesema kuwa, wakati Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipokuwa na matatizo makubwa zaidi ya kiuchumi, kisilaha na kijeshi, wananchi walisimama imara na kupambana ipasavyo katika kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu licha ya matatizo hayo yote.

Ayatullah Larijani amesema kuwa, Wamarekani wamekiuka makubaliano ya nyuklia ya Iran na nchi za kundi la 5+1 kwa kifupi JCPOA na kuongeza kuwa: Marekani inatumia mbinu nyingine za uhasa dhidi ya Iran na daima inapanua vikwazo vyake kwa taifa la Iran.

Mkuu wa Idara ya Mahakama hapa nchini amesisitiza kuwa, wananchi na viongozi wa Iran watatoa jibu kali kwa vitisho vya Wamarekani.

Katika upande mwingine Ayatullah Amoli Larijani amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haijali wala kuyapa umuhimu mashinikizo ya Marekani ya kutaka kuachiwa huru wahalifu wa nchi hiyo wanaoshikiliwa nchini Iran. Ameongeza kuwa: Iran ni nchi inayojitawala na inaendeleshwa kwa mujibu wa sheria zake na wala haitalegeza msimamo mbele ya mashinikizo ya Marekani. 

Afisa wa zamani wa FBI Marekani, Robert Levinson

Siku chache zilizopita Ikulu ya Rais wa Marekani White House, ilitoa taarifa iliyojaa vitisho ikitaka kuachiwa huru wafungwa wa nchi hiyo hapa nchini kwa majina ya Robert Levinson, afisa wa zamani wa FBI, na Siamak na Baquer Namazi.

Siamak na Baquer Namazi, Wairani ambao pia wana uraia wa Marekani, wamehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kwa kupatikana na hatia ya kushirikiana na dola adui la Marekani.