Aug 21, 2017 02:31 UTC
  • Jenerali Qassem Soleimani: Iran ni chemchemu ya uthabiti katika eneo

Kamanda wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema Iran haijawahi katu kuzusha mgogoro na kulea utakfiri; na leo hii imekuwa chemchemu ya uthabiti katika eneo la Mashariki ya Kati.

Jenerali Qassem Soleimani ameyasema hayo katika kikao cha 15 cha Siku ya Kimataifa ya Msikiti kilichofanyika hapa mjini Tehran na kusisitiza kuwa: Saudi Arabia imeanzisha makundi ya kigaidi yakiwemo ya Jaishul-Islam, Jaishul-Hur na mengineyo dhidi ya Iran, lakini hivi sasa Iran imekuwa chemchemu ya kupatikana uthabiti nchini Syria.

Jenerali Qassem Soleimani amesema, Iran imeweza kuvidhibiti vita vya kidini na kimadhehebu vilivyoanzishwa na Saudia katika eneo si kwa nguvu za kijeshi bali kwa nguvu za kidini na akafafanua kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inategemea nguvu na uwezo halisi usioweza kutetereshwa katika eneo.

Kikao cha 15 cha Siku ya Kimataifa ya Msikiti

Mkuu wa kikosi cha Quds cha Sepah, ameashiria kuuliwa shahidi Mohsen Hojaji na magaidi wa kitakfiri wa kundi la Daesh (ISIS) nchini Syria na kueleza kwamba shahidi huyo ni matunda ya malezi ya msikiti na akaongeza kuwa changamoto baina ya Iran na ulimwengu wa Magharibi ni juu ya msikiti ukiwemo Msikiti wa Al-Aqsa na Msikiti Mtukufu wa Makka.Jenerali Soleimani amesema msikiti ni maisha ya kidini, kisiasa na kijamii ya Ulimwengu wa Kiislamu na akasisitiza kwamba fitna za kimadhehebu na hujuma za madola ajinabi ni hatari mbili kubwa zinazoikabili Iran na Ulimwengu wa Kiislamu.../

Tags